KATIKA kona nyingi za jamii yetu, simulizi za uchungu, maumivu na ukimya zimeendelea kuwasibu wanawake na wasichana wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia na kuishia kupata mimba zisizotarajiwa.
Ukatili wa kijinsia si jambo geni tena. Wanawake wengi wameripotiwa kupigwa, kubakwa, kulazimishwa kufanya tendo la ndoa bila ridhaa yao, au hata kudhalilishwa kihisia. Haya yote huacha majeraha makubwa yasiyoonekana kwa macho, lakini yanayoendelea kuwasumbua kwa maisha yao yote, hasa pale linapoambatana na kupata mimba baada ya tukio.
Hata hivyo, licha ya Tanzania kuridhia Mkataba wa Maputo zaidi ya miaka 15 iliyopita, utekelezaji wa baadhi ya vipengele muhimu vya mkataba huo, hasa Ibara ya 14 inayohusu haki ya afya ya uzazi kwa wanawake, umeendelea kuwa changamoto kutokana na vikwazo vya kisheria, kijamii na kiimani.
Mkataba wa Maputo, ambao ni nyongeza ya Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu, unasisitiza haki ya wanawake kupata huduma salama za afya ya uzazi, ikiwemo huduma ya utoaji mimba katika mazingira yasiyosahihi kama vile ubakaji, mimba za maraimu, mimba hatarishi kiafya, au mimba za kulazimishwa.
Hata hivyo, sheria za Tanzania kupitia Kanuni ya Adhabu (Penal Code) kifungu cha 150, 152, 153 na 230, bado zinakataza utoaji wa mimba, isipokuwa pale tu inapolenga kuokoa maisha ya mama. Hali hii inaonekana kupingana na masharti ya Ibara ya 14 ya Mkataba wa Maputo.
Akizungumza na Michuzi Blog, mwanasheria Clay Shina, ambaye pia ni mdau wa haki za wanawake kutoka taasisi ya kijamii inayojihusisha na afya ya uzazi, alisema kuwa Tanzania haijafanya marekebisho ya sheria zake za ndani ili kuendana na matakwa ya Mkataba wa Maputo.
“Tunaposema Tanzania haijatekeleza mkataba huu, tunamaanisha kuwa bado haijabadilisha sheria ili kuwezesha upatikanaji wa huduma salama za afya ya uzazi kwa wanawake waliopo kwenye mazingira hatarishi,” alisema.

Kwa mujibu wake, changamoto kubwa inayozuia utekelezaji wa ibara hiyo ni mitazamo ya kijamii na imani za kidini ambazo haziruhusu utoaji wa mimba, hata katika hali za dharura.
“Katika dini ya Kiislamu hakuna shehe mwanamke msikitini, wala padri mwanamke kanisani. Lakini wanawake wanaruhusiwa kuongoza maeneo mengine. Hii inaonesha kuwa tunaweza kutafuta njia ya kati ili haki za wanawake zitekelezwe bila kuvunja misingi ya dini,” aliongeza.
Aidha, alieleza kuwa nchi kama Rwanda na Afrika Kusini tayari zimefanya mabadiliko ya kisheria kuruhusu utoaji wa mimba katika mazingira yaliyoainishwa na Maputo Protocol.
Rwanda, kwa mfano, inahitaji mwanamke kupata vyeti kutoka kwa madaktari wawili tofauti pamoja na idhini ya mahakama kabla ya kuruhusiwa kutoa mimba. Afrika Kusini imekwenda mbali zaidi kwa kuruhusu huduma hiyo hata kwa sababu za kiuchumi na kijamii.
“Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi hizo bila kuiga kila kitu. Tunaweza kuchukua kilicho bora kutoka Rwanda na Afrika Kusini na kukiweka katika mazingira ya nchi yetu,” alisema.
Mdau huyo aliongeza kuwa baadhi ya wanawake wana matatizo ya afya ya akili na hushindwa kulea watoto waliowazalia mitaani, huku wengine wakijifungua kutokana na ubakaji au mimba zisizotarajiwa bila kupata msaada wa kisheria wala wa kiafya.
Alitaja kampeni ya “Muache Asome” kuwa miongoni mwa mikakati inayoweza kusaidia wasichana waliopata mimba kurudi shule, lakini akasisitiza kuwa bila mabadiliko ya sheria na uhamasishaji wa jamii, mafanikio yatakuwa haba.
“Sheria inaweza kupitishwa, lakini ikashindwa kutekelezwa kutokana na hofu, imani potofu au ukosefu wa elimu kwa jamii,” alisema.
Amezitaka taasisi husika zikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Marekebisho ya Sheria na Wizara ya Afya kushirikiana kuhakikisha sheria zinahuishwa na utekelezaji wake unaenda sambamba na mkataba huo wa kimataifa.
Kwa mijibu wa Clay utafiti uliofanywa na taasisi ya Guttmacher Institute, World Health Organization (WHO), na pia African Union kupitia tathmini ya utekelezaji wa Maputo Protocol kuhusu afya ya uzazi barani Afrika umeonesha kuwa utekelezaji wa Maputo Protocol unaweza kupunguza zaidi ya asilimia 13 ya vifo vinavyotokana na mimba hatarishi au zisizotarajiwa.
Kisa cha Asha
Mmoja wa waathirika wa mimba isiyotarajiwa ni binti Asha Rahim kutoka Tanga, mwenye miaka 19, ambaye maisha yake yalibadilika kabisa alipobakwa na mjomba wake akiwa na umri wa miaka 16.
“Alikuwa mtu wa familia yetu, akitusaidia na mahitaji mara kwa mara. Siku moja nilipokuwa nyumbani peke yangu, alinibaka. Nilihisi kama dunia imenigeuka. Nilipata mimba. Mama alikasirika, baba alinifukuza. Nilihangaika hadi nilipopata msaada wa kituo cha wasichana waliotelekezwa,” anasimulia Asha huku akibubujikwa na machozi.
Leo hii Asha ni mama wa mtoto mmoja na hasomi tena. Hali yake ya kisaikolojia bado si ya kuridhisha. Anasema hampendi mtoto wake. Alijaribu kutoa mimba hiyo kwa kutumia njia za kienyeji bila mafanikio, akihofia kwenda hospitalini kwa kuogopa kukamatwa na kufunguliwa kesi.
Maoni ya Mtaalamu
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Kitaifa wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Sister Mgeni Kisesa, anasema endapo serikali itapitisha sheria ya kuruhusu utoaji wa mimba zisizotarajiwa, itawasaidia wanawake wanaopata mimba kutokana na ukatili wa kijinsia kama kubakwa au kulazimishwa.
“Kama sheria itaruhusu, tutaweza kuwasaidia wanawake wengi kuepukana na janga hili kwani kwa sasa, nchi yetu hairuhusu utoaji wa mimba isipokuwa ikiwa maisha ya mama yako hatarini,” alisema Kisesa.
Kisesa alieleza kuwa sheria hiyo pia itaokoa maisha ya wanawake wengi kwa kupunguza utoaji wa mimba usio salama.
“Mimba hizi zisizotarajiwa husababisha utoaji wa mimba usio salama, ambao una athari nyingi ikiwemo vifo vya asilimia 10 hadi 16 ya wanawake,” aliongeza.
Alisisitiza umuhimu wa wanawake waliobakwa kufika kituo cha afya ndani ya saa 72 ili kupata huduma stahiki kama vile dawa za kuzuia mimba na kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
“Kuna changamoto ya watu kuchelewa kufika kituo cha afya, hivyo kukosa huduma za kuzuia mimba,” alisema.
.jpeg)
Aidha, alieleza kuwa mwanamke aliyepata mimba isiyotarajiwa hawezi kwa sasa kupata huduma ya kutoa mimba kwa mujibu wa sheria, isipokuwa pale inapothibitishwa kuwa mimba inahatarisha maisha yake.
“Tunawashauri kuhusu athari za utoaji wa mimba usio salama, na kuwashauri kubaki na mimba hiyo. Hata hivyo, tunafahamu kuwa dunia ya sasa imejaa njia nyingi za kutoa mimba, na hivyo huwaambia warudi hospitalini endapo watapata matatizo,” alisisitiza.
Kisesa alihitimisha kwa kusema kuwa kupitishwa kwa sheria ya kuruhusu utoaji wa mimba kwa mazingira maalum kutasaidia kuokoa maisha ya wanawake wengi walioko hatarini.