Na. Nancy Kivuyo, MAKOLE
Jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 1 imetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo jumuishi la kutolea huduma za afya Kituo cha Afya Makole.
Kiasi cha shilingi 750,000,000 kimetolewa na serikali kuu na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma shilingi 289,794,329 zimelipwa kwa mkandarasi kwaajili ya ujenzi huo.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa wa mradi kwa Kamati ya Fedha na utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Kaimu Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Makole, Dkt. Salma Gwassa alisema kuwa ujenzi upo katika hatua ya msingi ‘foundation’ na wanatarajia mradi utakapokamilika wananchi wa Kata ya Viwandani na Jiji la Dodoma kwa ujumla watapata matibabu hapo.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutaleta ufanisi wa utoaji huduma za matibabu. “Mradi huu ukikamilika huduma za kliniki za kibingwa ‘speciality clinic’ zitapatikana, huduma za kiutawala zitaboreka na tutapanua wigo wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa nje na wa ndani” aliongeza Dkt. Gwassa.
Nae, Msimamizi wa mradi, Mhandisi Ntezimana Chongele alisema kuwa mradi upo katika hatua nzuri na utatekelezeka kwa wakati. “Napenda kuwahakikishia kuwa mkandarasi yupo vizuri, eneo hili lina asili ya maji kama mnavyoona amefanya kazi kubwa kuyavuta na anatarajia kuendelea na ujenzi kwa kasi kuhakikisha anamaliza mradi ndani ya muda uliopangwa” alisema Mhandisi Chongele.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi Jiji la Dodoma, Joan Mazanda aliisisitiza kamati ya mradi kusimamia vizuri mradi huo ili ukamilike kwa wakati wananchi wapate huduma za matibabu. “Kituo cha Afya Makole kinatoa huduma za afya nzuri sana, tunategemea ujenzi ukikamilika wananchi watapata huduma nzuri. Nawasisitiza kusimamia vilivyo mradi huu, fedha iliyotolewa ni nyingi tutafurahi kuona unakamilika kwa viwango vile tunavyotarajia” alisisitiza Mazanda.
Mradi wa ujenzi wa jengo jumuishi la kutolea huduma za afya Kituo cha Afya Makole unatarajiwa kukamilika tarehe 27 Januari, 2026 na unatarajia kuhudumia wananchi 95,320 kwa mwaka.