Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Edna Kajuna akimuelezea huduma za upasuaji wa moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo mtaalamu wa kliniki ya kadi Klabu ya Young African (Yanga) Haji Omary almaarufu kama mzee mpili alipotembelea banda la Taasisi hiyo leo katika maonesho ya wiki ya Afya Zanzibar yanayoendelea katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Airport.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva Wakuganda akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) mtoto aliyefika katika banda la Taasisi hiyo kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya wiki ya Afya Zanzibar yanayofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Airport.
Mratibu wa utalii matibabu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya wiki ya Afya Zanzibar yanayofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Airport.
Picha na: JKCI
Na: Mwandishi maalumu – Zanzibar
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inashiriki katika maonesho ya wiki ya afya Zanzibar kwa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi bila gharama.
Maonesho hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Airport yatawawezesha wananchi kupata fursa ya kuchunguza afya zao na kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wameishukuru Serikali yao kwa kuanzisha maonesho hayo yanayotoa fursa kwa wananchi wake kupata huduma bobezi za afya bila gharama.
Mariam Suleiman mkazi wa Zanzibar alisema maonesho hayo yameweza kutoa fursa kwa watoto wake kupimwa moyo bila gharama kwani alikuwa na wasiwasi kuhusiana na afya za watoto hao.
“Hapa nilipo nimetoka wodini hivi karibuni, watoto wangu hawa mapacha wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo la kubanwa kifua na daktari alinishauri nikipata nafasi niwapime moyo, kama bahati leo wamepimwa. Naishukuru sana Serikali yangu kwa kufanya maonesho haya na kutupa fursa ya kuchunguza afya bila gharama”, alisema Mariam
Naye Ibrahimu Mohamed mkazi wa Zanzibar alisema Serikali imeona umuhimu wa wananchi wake kupata huduma za uchunguzi wa afya hivyo kushirikisha Hospitali za kibingwa ili waweze kuchunguza magonjwa kama ya moyo ambayo mara nyingi watu hawapimi.
“Tunawashukuru pia wataalamu ambayo mmetumia muda wenu kufika hapa kwa ajili yetu, tunaomba huu mwanzo mliouanzisha mwaka huu usiishie hapa bali muendele mara kwa mara kutupa elimu na kutufanyia uchunguzi”, alisema Ibrahimu
Sambamba na kutoa huduma za elimu na uchunguzi wa magonjwa ya moyo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maonesho hayo pia imeishirikisha na Shirika lisilo la Kiserikali la Heart Team Afrika Foundation (HTAF) kuihamasisha jamii kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.