Na Silivia Amandius
Bukoba.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, ameongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe ngazi ya jamii kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025. Kikao hicho kimefanyika Aprili 9, 2025, katika ukumbi wa makao makuu ya Halmashauri, kikihusisha waganga wafawidhi, maafisa lishe, na watendaji wa kata.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Mhe. Sima aliwapongeza walimu na shule kwa kuanzisha bustani za mboga na kupanda miti ya matunda kama sehemu ya kuboresha lishe kwa wanafunzi. Alisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto ya utapiamlo, hasa katika kata zinazoathirika zaidi.
“Lazima tupige vita lishe duni katika Halmashauri yetu kwa kuhakikisha viashiria vyote vya lishe vinafikiwa, ikiwemo utoaji wa chakula mashuleni kwa asilimia 100,” alisema Mhe. Sima.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Wilaya, Bi. Janeth Mahona, aliwasilisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi husika. Mafanikio hayo ni pamoja na upatikanaji wa mashine tatu za kurutubisha unga katika Kata ya Kemondo, mafunzo ya matibabu ya utapiamlo, matibabu ya watoto sita waliokumbwa na utapiamlo katika hospitali ya wilaya, na mafunzo ya uchakataji wa soya kwa wanawake 49. Pia, alieleza kuhusu uendelezaji wa vitalu vya lishe katika shule mbalimbali.
Hata hivyo, Bi. Janeth alibainisha changamoto kadhaa, zikiwemo ucheleweshaji wa taarifa za lishe kutoka kata nyingine na baadhi ya wanafunzi kutopata chakula shuleni.