Waziri ofisi ya Rais menejimenti ,utumishi wa Umma na utawala bora Boniface Simbachawene akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha.

Rais wa chama hicho Boniface Mwabukusi akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha leo


……….
Happy Lazaro,Arusha .
Waziri ofisi ya Rais menejimenti ,utumishi wa Umma na utawala bora Boniface Simbachawene ametaka kuwepo kwa ushirikiano kati ya vyama vya siasa, taasisi za kisheria, na wananchi katika kujenga utawala bora ambapo amepongeza TLS kwa mchango wake katika masuala ya kisheria na utawala bora.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua mkutano mkuu wa chama cha sheria Tanganyika ( TLS) unaofanyika mkoani Arusha .
Aidha amesema kuwa chama hicho ni muhimu katika kutoa miongozo ya kisheria na kuhamasisha demokrasia.
Simbachawene amesema ,kutokana na mabadiliko yanayoendelea ndani ya vyama vya siasa ni muhimu kuzingatia maoni ya wananchi katika mabadiliko ya katiba na sheria.
Aidha amefafanua kuwa ,mawazo ya kuboresha siasa nchini ni mazuri huku akiahidi kushirikiana na TLS katika juhudi za kuboresha mifumo ya kisheria na utawala bora.
Kwa upande wake wa Rais wa chama hicho Boniface Mwabukusi amesema kuwa ,chombo hicho kinapaswa kuwa na mamlaka kamili, uhuru wa kiutendaji, na uwezo wa kutoa maelekezo yenye uzito sawa na amri za mahakama.
Aidha chama hicho kimeishauri Serikali kuanzisha chombo maalum kitakachowezesha wananchi kuwasilisha na kufuatilia kwa ufanisi malalamiko yao, hususani yanayohusu haki za binadamu na utawala bora.
Amesema kuwa mkutano wao wa mwaka unaongozwa na kauli mbiu isemayo “uchaguzi na utawala wa sheria :wito wa uangalizi wa kisheria na uwajibikaji katika mfumo wa uchaguzi wa Tanzania “.
Amebainisha kuwa kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa misingi ya utawala wa kisheria inazingatiwa katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kuanzia Maandalizi ,upigaji kura, hadi utoaji wa matokeo kwani hii inafanya watafakari wajibu wao kama wanasheria na viongozi wa kitaaluma katika kulinda haki ya wananchi ,kudumisha amani ,na kuimarisha demokrasia.
“Katika kipindi hicho cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 tunakumbushana kuwa uangalizi wa kisheria si hiari bali ni wajibu na uwajibikaji na ni msingi wa uongozi bora ,na TLS inaamini kuwa kwa kushirikiana na serikali ,mahakama ,tume huru ya uchaguzi ,vyombo vya ulinzi na usalama ,pamoja na wananchi tunaweza kuhakikisha uchaguzi wa haki huru na kuaminika” amesema .
Amesema kutokana na kauli mbiu hiyo inayoakisi dhamira ya TLS kuhakikisha kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa msingi wa kisheria,haki ,uwazi , na uwajibikaji ,wanatambua kwamba wanasheria wanao wajibu wa kipekee katika kulinda haki ya wananchi na kutetea misingi ya katiba yetu hasa katika kipindi hichi cha kuelekea katika uchaguzi mkuu na pia wanatambua wana wajibu wa kulinda utawala wa sheria kwa wananchi pamoja na kishirikiana na serikali katika maswala ya kisheria yanayolenga ustawi wa jamii na ushiriki wao si tu kwa serikali bali ni dhati unaotokana na dhamira ya kuona haki inapatikana kwa wote.
Aidha ameseema kwa kuzingatia hali halisi ya utendaji kazi wa vyombo vya utoaji haki hususan ni jeshi la polisi na kwa kuzingatia mazingira ya kiusalama kwa raia na kukithiri kwa kitendo vya utekaji na kupotezwa kwa wananchi TLS inatoa rai kwa serikali kuunda chombo maalum cha kisheria kitakacho simamia na kuangalia namna ambavyo wananchi wanatendewa haki ili kuwa na daraja la wananchi kufikisha malalamiko yao
Amebainisha kuwa TLS itaendelea kushirikiana na serikali kwa karibu kuhakikisha kuwa mfumo wa uchaguzi na haki nchini unazingatia viwango vya juu vya sheria , maadili ,na haki kwa wote na wanaamini kwa ushirikiano huo wataendelea kujenga taifa lenye haki sawa kwa wote na demokrasia imara.