Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja kulia,akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri baada ya kufungua mkutano wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Mbinga(Mbifacu)katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga,katikati aliyekuwa Mfilisi wa Mbifacu Watson Nganiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Peres Magiri kushoto,akisamiliana na Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa Wilaya ya Mbinga Faraja Komba baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga,katikati Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mkoani RuvumaPeres Magiri katikati akiwa kwenye Picha ya pamoja na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja wa pili kulia,Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbinga(Mbifacu)Fraja Komba kulia na Mwenyekiti wa Chama hicho Micheal Kanduyu wa pili kushoto mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu 23 wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga.
Baadhi ya Viongovi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika(Amcos)kutoka Wilaya ya Mbinga na Nyasa wakifuatilia Mkutano Mkuu wa 23 wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbifacu jana.
Maafisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga,Halmashauri ya mji Mbinga Nyasa wakifuatilia Mkutano Mkuu 23 wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbinga Mbifacu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga.
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
MKUU wa Mkoani Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,amewaonya Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika(Amcos) katika Mkoa huo kujiepusha kutorosha na kununua kahawa kwa njia ya magendo kwani Serikali itawachukulia hatua kali kwa kuwa vitendo hivyo vinachangia kuhujumu uchumi wa Mkoa huo.
Kanali Abbas,ameviagiza vyombo vyote vya dola kuwashughulikia Viongozi wa Amcos na makampuni yatakayonunua kahawa ikiwa changa mashambani kwa sababu kufanya hivyo ni kuwanyonya Wakulima na kurudisha nyuma maendeleo.
Ametoa kauli hiyo jana katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri kwenye Mkutano Mkuu 23 wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Mbinga(Mbifacu )uliofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga.
Aidha,amepiga marufuku wakulima kuuza kahawa kwa walanguzi na kusisisitiza kuwa,Vyama vya msingi vya Ushirika na vyama vikuu ndiyo vyenye jukumu la kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima na kupeleka kwenye minada kwa ajili ya kununuliwa na makampuni yatakayojitokeza kwa kushindanisha bei katika soko la Dunia.
“Ni marufuku Viongozi wa vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)makampuni na watu binafsi kununua na kuuza kahawa kwa njia ya magendo,viongozi wa Amcos mnatakiwa kusimamia agizo hili kwa ajili ya kulinda haki ya mkulima”alisema.
Alisema,Serikali imeandaa utaratibu wa kushindanisha kampuni ili kununua kahawa mnadani baada ya wakulima kukusanya kahawa kupitia vyama vyao vya ushirika na kulipwa fedha taslimu huku wakisubiri nyongeza kutokana na faida itakayopatikana.
Badala yake,amewataka viongozi wa Amcos kwenda kuimarisha ushirika ili uweze kuleta tija kwa Wakulima na kuepuka kuhujumu sekta ya ushirika ambayo ni uti wa mgongo kwa wakulima na chombo cha maendeleo kinachochea na kuimarisha uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Abbas alisema,Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega kwa kuhakikisha sekta ya ushirika inaendelea kuimarika kwa sababu ni sekta muhimu kiuchumi wa Mkoa wa Ruvuma.
Katika nasaha zake Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh.bilioni 200 hadi kufikia Sh.bilioni 900 msimu wa kilimo 2024/2025.
Amewaomba Wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika,kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kutoa pembejeo hasa mbolea za ruzuku kwa wakulima ambazo zimewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la kahawa.
Meneja Mkuu wa Mbifacu Faraja Komba alisema,ili kuweza kutekeleza shughuli mbalimbali za Chama katika msimu 2024/2025 Mbifacu imefungua kampuni ya ununuzi na uuzaji wa kahawa yenye jina la MBIFACU COMPANY LTD kwa ajili ya kununua kahawa katika Soko la awali la mnada na kuuza kwenye soko la nje.
Alisema,bodi inaamini kuwa mradi huo wa Kampuni utaongeza chachu ya ushindani wa bei kwa mkulima katika masoko hayo na kuongeza mapato ya Chama.
Komba alisema,ili kufanikisha mpango huo Mbifacu imepanga kutumia Sh.1,282,099,800 na kati ya hizo Sh.bilioni 1,140,328,200 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali Sh. 319,300,000 kwa ajili ya miradi ambapo Sh.115,890,060 zitatumika kumalizia ukarabati wa awamu ya kwanza block 3 katika Hoteli ya Mbicu.
Mwenyekiti wa Mbifacu Micheal Kanduyu,ameiomba Serikali kuendelea kuwabana watumishi wa umma wanaotumia mwamvuli wa makampuni ya kiuni kununua kahawa kwa njia ya magendo kwa kuwa wanachangia sana kuongezeka kwa wafanyabiashara wasiozingatia sheria za ushirika.
Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja, ametoa wito mzito kwa Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika chini ya mwamvuli wa MBIFACU kuhakikisha wanasimamia wajibu wao ipasavyo, wakiepuka uzembe, migogoro, na vitendo vya kuhujumu uchumi wa wakulima.
Muhoja amesisitiza umuhimu wa ubora wa kahawa, uwajibikaji wa viongozi, na usimamizi madhubuti wa uingiaji wa mikataba ya uuzaji wa Kahawa.
Muhoja ameeleza kuwa, baadhi ya Vyama vimekuwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kutowalipa wakulima kwa wakati na Viongozi kutotekeleza majukumu yao ipasavyo huku Soko la awali linalofanyika kupitia Mikataba limegeuzwa kuwa kichaka cha kuweka bei zisizo rasmi kwa manufaa binafsi.