Wazazi na walezi wametakiwa kuwalea watoto wao kwa kuzingatia maadili mema na kuhakikisha wanadhibiti matumizi ya simu na teknolojia nyingine, ambazo zinatajwa kuwa na madhara makubwa endapo zitatumiwa bila udhibiti.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 12 ya Shule ya Msingi Waja, Mkurugenzi wa Makampuni ya Waja, Chacha Wambura, alisema kuwa ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yanayowajenga kuwa raia wema. Aliongeza kuwa matumizi mabaya ya simu na teknolojia, hasa mitandao ya kijamii, yanaweza kuwa chanzo cha tabia zisizofaa miongoni mwa watoto.
“Mazingira ya sasa yanahitaji wazazi kuwa makini zaidi. Tunapaswa kuwaelekeza watoto wetu matumizi sahihi ya teknolojia ili kuepuka madhara yanayoweza kusababisha athari mbaya kwa ukuaji wao,” alisema Chacha Wambura.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, alieleza kuwa shule za Waja zimeendelea kuwa mfano mzuri katika kutoa elimu bora na kuwalea watoto katika misingi ya maadili. Aliwasisitiza wazazi kuendelea kushirikiana na shule ili kufanikisha lengo hilo.
“Shule hizi zimeweka mikakati mizuri kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na nidhamu pamoja na kupata elimu iliyo bora, ambayo itawasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Mohamed Gombati.
Naye Mkurugenzi wa Shule za Waja, Jackline Tesha, alisema shule hiyo imejikita katika kuwalea watoto kimaadili na kutoa elimu bora inayowajenga wanafunzi kuwa raia wema na viongozi wa baadaye.
Maoni ya Wazazi Baadhi ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo walitoa maoni yao kuhusu matumizi ya simu kwa watoto. Godfrey Noel, mzazi mmoja, alisema kuwa udhibiti wa matumizi ya simu ni muhimu ili kuhakikisha watoto wanajikita katika masomo na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwapotosha.
“Mazoea ya watoto kutumia simu hasa wakiwa shuleni ni jambo ambalo linahitaji kudhibitiwa mapema kwa ajili ya mustakabali mzuri wa watoto wetu,” alisema Noel.
Rahel Anthony, mzazi mwingine, aliongeza kuwa wazazi wanapaswa kujihusisha zaidi na maisha ya watoto wao na kuhakikisha wanatumia teknolojia kwa manufaa badala ya kuwaacha kutumia simu bila udhibiti.
Mahafali hayo yalienda sambamba na dua maalum kwa ajili ya shule hiyo, huku wazazi na walimu wakiahidi kushirikiana katika kuwalea watoto kimaadili na kitaaluma.