…………….
Na Sixmund Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kutatua changamoto za muingiliano kati ya binadamu na wanyamapori kwa kutoa mafunzo maalum kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa kufunga Kozi Maalum Na. 22/2025 ya VGS katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii – Likuyu Sekamaganga, mkoani Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi (ACC), Hadija Malongo, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ushiriki wa jamii katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi.
“Ni matumaini yangu kuwa mbinu mlizojifunza mtazitumia kwa weledi mkubwa katika maeneo yenu. Tunahitaji askari waaminifu na waadilifu watakaosaidia kulinda maisha ya wananchi, mali zao na rasilimali za taifa,” amesema Kamishna Malongo.
Aidha, amepongeza chuo hicho kwa mchango wake mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za maliasili, na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kukiunga mkono ili kiweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo, ACC Japhary Lyimo, amesema kuwa wahitimu wamepata stadi mbalimbali zikiwemo za usimamizi wa rasilimali, mwitikio wa haraka kwa changamoto za wanyamapori, pamoja na ulinzi wa chakula, watu na mali katika maeneo ya vijijini.