Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli, jijini Dar es Salaam ambaye alifika kujitambulisha.
Katika kikao hicho, Mhe. Kikwete amesema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa Serikali ya Uswisi kupitia shirika la Swiss Aid kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, maendeleo ya jamii pamoja na masuala ya ukuzaji ujuzi kwa vijana.
Aidha, Waziri Kikwete amepongeza ubalozi wa Uswisi kwa mchango wake katika kufanikisha kukamilika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024 ambayo inatoa mwongozo kwa vijana na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi hapa nchini, Mhe. Nicole Providoli amesema kuwa Uswisi itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili Sera hiyo mpya ya vijana toleo la 2024 inawafikia vijana wengi.