Johannesburg, May 2025– Baada ya mchakato mpana wa uwasilishaji wa mapendekezo ya ubia, Airtel Africa imeiteua rasmi Publicis Groupe Africa kuwa mshirika wake wa masoko ya pamoja katika masoko 12 muhimu barani Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania. Ushirikiano huu wa kimkakati unaashiria hatua kubwa katika maendeleo ya masoko barani Afrika, ukileta pamoja taasisi mbili zenye nguvu na maono ya pamoja ya kutoa huduma za kibunifu zinazotegemea data, zenye mvuto kwa hadhira mbalimbali za bara hili.
Ushirikiano huu utatekelezwa katika nchi zifuatazo: Congo Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Niger, Chad, Gabon, Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania, Zambia, Malawi na Madagascar, huku majadiliano yakiendelea kuhusu masoko mengine.
“Ushirikiano huu si tu kielelezo cha ushindi kwa Publicis Groupe Africa, bali pia ni ushuhud wa aina mpya ya masoko bila mipaka — ya ushirikiano wa kweli na wa kuangalia mbele kwa mustakabali wa Afrika. Tunathamini sana imani ambayo Airtel imetupa na tunatazamia kushirikiana kwa karibu katika kujenga chapa yenye athari kubwa na ya maana kwa bara letu,” alisema Koo Govender, Mkurugenzi Mtendaji wa Publicis Groupe Africa.
Airtel Africa, ni kampuni inayoongoza kwa kutoa huduma za mawasiliano na kifedha, inayofanya kazi kwa malengo mahususi ya kubadilisha maisha ya watu kwa kuwaunganisha wale wasiokuwa na mawasiliano, kuwafikia watu wenye uhaba wa huduma za kifedha na pia kuziba ufa wa kidijitali katika maeneo inapotekeleza operesheni zake. Kujidhatiti kwakampuni hiyo katika uvumbuzi, ujumuishaji na upatikanaji wa huduma ndio umeifanya iwe ni chapa yenye matokeo makubwa.
Kwa kuchochewa na dhamira ya pamoja ya kuwa wabunifu, wenye ushirikiano wa karibu na wanaozingatia muktadha wa kila soko, Publicis Groupe Africa, kupitia tawi lake la The Partnership Africa lililopo Nairobi, liliwasilisha mkakati bora unaojumuisha mbinu za kibunifu, hadithi zenye mvuto, usimamizi wa vyombo vya habari, suluhisho za kidijitali na matumizi ya data ili kuunga mkono malengo ya muda mrefu ya Airtel.
Kupitia mtandao wake wa washirika barani Afrika, ushirikiano huu utawezesha utekelezaji wa kampeni muhimu kwa uwanda mpana kwenye kila soko, pamoja na kutunza tofauti za kitamaduni na kuzingatia ushiriki wa jamii.
Ushirikiano huu ni ishara ya dhamira ya muda mrefu ya Airtel Africa katika kubadilisha namna inavyowasiliana na kushirikiana na jamii na wateja wake kote barani Afrika.