Na Fredy Mgunda, Lindi.
Serikali ya Mkoa wa Lindi imewapokea rasmi madaktari bingwa 47 chini ya mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, awamu ya tatu, kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika hospitali zote za wilaya ndani ya mkoa huo.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, alisema kuwa ujio wa madaktari hao ni sehemu ya jitihada za serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hasa wale walioko maeneo ya vijijini ambako awali walilazimika kusafiri mbali kupata huduma za kibingwa.
“Huduma hizi zitapatikana katika maeneo saba ndani ya mkoa kwa siku sita mfululizo kuanzia leo. Lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na kwa wakati,” alisema Bi. Omary.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuboresha sekta ya afya kwa kujenga miundombinu ya kisasa, kununua vifaa tiba vya kisasa, pamoja na kuongeza wataalamu mbalimbali wa afya nchini.
Kwa upande wake, Mratibu wa timu hiyo ya madaktari, Michael Mbele, alieleza kuwa madaktari hao wamejipanga kikamilifu kutoa huduma zote muhimu za afya kwa wananchi wote, bila ubaguzi, katika hospitali za wilaya walizopangiwa.
“Tumewakilishwa na wataalamu wa kada zote za afya, kuanzia magonjwa ya ndani, watoto, wanawake, upasuaji na hata huduma za kisaikolojia. Huduma zote hizi sasa zitapatikana katika hospitali za wilaya,” alisema Mbele.
Wananchi wa Mkoa wa Lindi waliopata fursa ya kuhudumiwa walieleza furaha na shukrani kwa serikali, hususan kwa Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini, hatua ambayo wameitaja kama ya kipekee na ya kupongezwa.