Na Sophia Kingimali.
Siku ya wakulima wa NOURISH imeendelea katika wilaya 10 ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Iramba, wakilenga kutoa elimu kwa wakulima wanufaika wa mradi pamoja na jamii nzima ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo na elimu ya lishe, usafi wa mwili na mazingira pamoja na kushiriki katika miradi mbalimbali ambayo itawasaidia kuongeza kipato
Lakini pia,inatoa fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye mashamba ya mfano yaliyofanikiwa, kuunganishwa na biashara za kilimo, na kuongeza maarifa kupitia mapishi yenye lishe bora.
Akizungumza katika Siku ya Wakulima wa NOURISH iliyofanyika Kijiji cha Ngalagala, Kata ya Kinampanda, Wilaya ya Iramba, Afisa wa mradi wa NOURISH, Bi. Salome James, amesema licha ya mafanikio makubwa katika mwaka mmoja, wakulima wamekumbana na changamoto za upungufu wa mvua kutokana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na miundombinu duni ya barabara inayozuia upatikanaji wa pembejeo kwa wakati.
Aidha ameendelea kusema kuwa mradi unaendelea kutoa suluhisho endelevu ili kusaidia wakulima pia mradi wa NOURISH umefanikiwa upimaji wa afya ya udongo kwenye mashamba 320, kuwawezesha wakulima kujua ubora wa ardhi zao.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Afisa Tarafa Charles Makala alisisitiza umuhimu wa wakulima kutekeleza mbinu za kilimo walizojifunza, huku akihimiza maafisa ugani kushirikiana kwa karibu na wakulima ili kuhakikisha teknolojia za NOURISH zinatumika kikamilifu.
“Vikundi vya wakulima, panueni ushirikiano, sajilini rasmi, na endeleeni kushirikiana kwa maendeleo ya pamoja. Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha kuwa juhudi zilizowekezwa hazipotei bali zinazaa matunda ya kudumu katika jamii zetu.”amesema.
Mpaka sasa, maadhimisho ya Siku ya Wakulima wa NOURISH yamefanyika katika wilaya za Momba, Mkalama, Mpwapwa, Sumbawanga, Kalambo, Hanang, na Mbozi, huku ukitarajia kuendelea kujenga ustahimilivu wa wakulima na kuimarisha sekta ya kilimo kwa maendeleo endelevu.
Mradi wa NOURISH Tanzania (Kuwawezesha Wakulima Wadogo kwa Usalama wa Chakula na Ustahimilivu wa Tabianchi) ni mradi wa miaka mitano (2024-2028) unaolenga kufanikisha usalama wa chakula unaozingatia ustahimilivu wa tabianchi kwa watu 168,000, wakiwemo wakulima wadogo, biashara ndogo na za kati (MSMEs), na vikundi vya wakulima katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Rukwa, Singida, na Songwe. Kwa kuzingatia minyororo minne ya thamani yenye uwezo mkubwa (mtama, alizeti, maharage, na mboga mboga), mradi unashughulikia changamoto za usalama wa chakula kwa wakulima wadogo kupitia njia tatu kuu za mafanikio ambazo ni Kuongeza uzalishaji kupitia mafunzo ya kilimo kinachozingatia tabianchi, upatikanaji wa pembejeo bora, na rasilimali za kifedha.
Pia,Kuimarisha masoko ya chakula kwa kushirikisha wadau wa biashara, kutumia suluhisho za kidijitali, na kuwawezesha wakulima wadogo na MSMEs.
Aidha Kuboresha matumizi ya rasilimali za kaya kwa kuhamasisha mlo wenye lishe bora, bajeti ya chakula cha kaya, na kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kaya.
Mradi unafadhiliwa na Shirika la maendeleo la Norway (Norad) na kutekelezwa kwa ushirikiano wa SNV, Farm Africa, T-MARC, RECODA, na MIICO