Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CP Awadhi Juma Haji akizungumza wakati wa ziara hiyo

Fred Mfikwa Mkuu wa kitengo cha usalama GASCO
**
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CP Awadhi Juma Haji, ameongoza Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara—mikoa inayopitiwa na miundombinu ya gesi asilia na kufanya ziara ya ukaguzi wa miundombinu hiyo inayotoka Msimbati, Madimba hadi Kinyerezi kupitia Somanga.
,Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya GASCO inayosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, CP Awadhi amebainisha kuwa Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuhakikisha miundombinu ya gesi asilia inakuwa katika hali ya usalama wa kutosha, kwa kuwa rasilimali hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Jeshi la Polisi lina makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya GASCO kupitia TPDC kwa ajili ya kutoa ulinzi kwenye miundombinu ya gesi asilia. Ziara hii ni utekelezaji wa takwa la makubaliano hayo, ambapo kila mwaka tunatakiwa kufanya ukaguzi ili kutathmini hali ya kiusalama,” amesema CP Awadhi.
Amesema ukaguzi huo unaangazia tathmini ya hali ya usalama katika kipindi kilichopita, kutambua changamoto zilizojitokeza na namna zilivyoshughulikiwa, pamoja na kupanga mikakati ya kuimarisha zaidi ulinzi wa miundombinu hiyo.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru wenzetu wa GASCO na TPDC kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kuandaa ziara hii. Ushirikiano huu unatupa nafasi ya kufanya tathmini ya pamoja ya hali ya kiusalama kwenye maeneo yote ya miundombinu ya gesi asilia,” ameongeza.
Aidha, naye Bw. Fred Mfikwa ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Usalama GASCO, ameeleza kuwa mbali na vyombo vya dola, GASCO pia imeingia mikataba na vijiji vinavyopitiwa na miundombinu hiyo, ambapo wananchi hushiriki katika shughuli za ulinzi na usafi wa maeneo yanayopitiwa na miundombinu ya gesi asilia.
Mfikwa amesema hatua hii imeongeza urafiki kati ya TPDC na jamii, hali inayowasaidia kupokea taarifa muhimu za kiusalama na kutambua mapema hitilafu zinazoweza kutokea.
Aidha, ametoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa namna lilivyo mstari wa mbele katika kushughulikia changamoto za kiusalama.
“Kwa kipindi chote tangu tuingie makubaliano na Jeshi la Polisi, hatujakumbwa na changamoto yoyote kubwa. Polisi wamekuwa wakijitokeza haraka tunapohitaji msaada, na hatua za kisheria huchukuliwa kwa wanaoharibu au kuingilia miundombinu yetu,” amesema.