NA DENIS MLOWE, IRINGA
VIJANA nchini hususani wanavyuo wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani na utulivu na kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Wito huo umetolewa na Mdau wa Maendeleo na mwanasiasa anayekuja juu mkoani Iringa, Shalom Robert wakati akizungumza na Umoja wa Vijana wa Ccm Tawi la chuo Kikuu cha Iringa na kufanyika katika ukumbi wa Ccm kata ya Kihesa.
Shalom ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo alsema wakati tukielekea katika uchaguzi mkuu kuna kuwepo na vitendo mbalimbali viovu ikiwemo rushwa hivyo ndio wakati wa vijana kupambana navyo na kuviepuka na kudumisha utulivu na amani.
“Naombeni twendeni tukaepuke rushwa kwasababu Kuna mambo kadha wa kadha huwa yanatokea Katika kipindi hiki Vijana twendeni tukapinge hayo mambo maovu lakini twendeni tukamsikilize yule mwenye sera ambaye yupo tayari kutuongoza”
Aidha Shalom ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kuboresha na kutekeleza miradi mbalimbali hususani Sekta ya Elimu .
Aidha aliwataka vijana kuwa wazalendo katika nchi yao na kuyasemea mazuri shughuli zinazofanywa na serikali na kuwaepuka wanasiasa ambao wamekuwa wakipinga kila kitu kinachofanywa na serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema uzalendo si gharama kubwa bali ni kujitoa kwa dhati kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Ndugu zangu, kuwa wazalendo katika nchi yetu si gharama kubwa ni moyo wa kujitoa na kuwa na imani kubwa kwa viongozi wetu wa nchi Lakini pia ni lazima mzitambue na kuzitumia kwa vitendo fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yenu ili muwe msaada mkubwa kwa jamii,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa katika sekta ya elimu wanavyuo wamefaidika kwa kiasi kikubwa na mikopo inayotolewa na serikali na kuwataka wanavyuo kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwani wengi wamesoma bila usumbufu ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“Kipindi Cha nyuma tumeshuhudia Vyuo Vikuu Wanafunzi wengi walikuwa wanaleta migomo lakini tangu ameingia Rais Samia hakuna mgomo wowote uliotokea kwenye vyuo” Alisema
Kwa upande wao wanavyuo hao wamemshukuru Shalom kwa kuweza kuwa msaada mkubwa wa ujenzi wa ofisi ya umoja wa vijana wa CCM na kuahidi kumuunga mkono Rais kwa kumpa kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.