Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara imeanza rasmi kutoa huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, baada ya Bohari ya Dawa(MSD) Kanda ya Kilimanjaro kukamilisha kufunga mashine sita (6) kwa ajili ya huduma hiyo.
Meneja wa MSD Kanda ya Kilimanjaro Rehema Shelukindo ameeleza kuwa mashine hizo sita ni za awali, na mashine nyine nne zitaongezwa baadaye kadri mahitaji yatakavyoongezeka.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dokta Yesige Mutajwaa ameishukuru wizara ya Afya kupitia MSD kwa kununua na kusimika mashine hizo katika hospitali hiyo, kwani zitasaidia kuimarisha afya za wananchi Mkoani humo, ikiwemo kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo mikoa ya jirani.
Amesema tayari huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo katika hospitali hiyo zimeanza na mgonjwa wa kwa kwanza ametoka salama.