Na Mustapha Seifdine, Karatu.
Katika kuhakikisha mazingira ya hifadhi na shoroba za Wanyamapori yanabaki salama kwa uhifadhi endelevu, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) imeendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi wa vijiji vinavyopakakana na hifadhi ya Ngorongoro kupambana na mmea vamizi hatari uitwao Gugu Karoti (Parthenium hysterophorus) ambao umeota baadhi ya maeneo.
Hatua ya ushirikishaji wa jamii ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kudhibiti mimea vamizi nchini, hususan katika maeneo ya yaliyohifadhiwa na kuzilinda shoroba muhimu zinazounganisha mifumo ya ikolojia kama vile shoroba ya Upper Kitete inayounganisha hifadhi za Ngorongoro, ziwa Manyara na Tarangire.
Afisa Uhifadhi darala la Kwanza Gregory Mtega kutoka NCAA akiongoza wananchi wa Kijiji cha Upper Kitete na baadhi ya wataalam ameeleza kuwa operesheni ya kung’o gugu karoti imefanyika kwa mafanikio makubwa kupitia ushirikiano kati ya NCAA, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na shirika la PAMS na kuongeza kuwa juhudi hizo zinaendelea katika vijiji vingine vinavyopakana na hifadhi kwa ajili ya kuhifadhi uoto wa asili, malisho ya mifugo, na maisha ya wanyamapori.
“Tumekuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya uhifadhi shirikishi kwa wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi, NCAA kila mwaka tunatoa miche ya miti bure wananchi wapande kwenye maeneo yao, tunagawa mizinga ya Nyuki kuwainua kiuchumi na kupambana na Wanyama wanaoingia kwenye maeneo hayo, pamoja na programu hizo tumeamua pia kuwahusisha kwenye kung’oa mimea vamizi ili kulinda mfumo wa ikolojia kuwa imaraa, kuimarisha nyanda za malisho na kuwa na uhifadhi endelevu”
Mtega ameongeza kuwa Gugu Karoti ni mmea unaosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kuwa unazaliana kwa kasi (mbegu zaidi ya 40,000 kutoka mmea mmoja!), na ni tishio kwa wanyamapori, mifugo, na hata kilimo cha wananchi hivyo mamlaka imewekeza juhudi za kutosha kukabiliana nalo kw akutumia njia mbalimbali.
Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Kornelio Lengai, amepongeza ushirikiano wa NCAA na kueleza kuwa mmea huo umekuwa kikwazo kwa uzalishaji wa chakula na maisha ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hivyo Jitihada za NCAA kushirikiana na wadau mbalimbali ni ishara nzuri katika uhifadhi endelevu kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Emanuel Siriri, mkazi wa kijiji cha Upper Kitete, ameishukuru NCAA kwa kuendelea kutoa elimu na kuwashirikisha wananchi wa kijiji hicho ambapo jitihada hizo si tu zinaleta matumaini bali zimefungua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia kazi za udhibiti wa mmea huo ambao unapodhibitiwa unaboresha shughuli za kilimo na kupata mazao ya kutosha.