Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa onyo kali kwa mtu yeyote kutamka neno lolote bila ruhusa rasmi ya Mahakama baada hakimu kuwa ameshaingia mahakamani.
Hatua hiyo imekuja kufuatia tukio la mshtakiwa ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kuingizwa mahakamani kisha akanyoosha mkono juu na kutamka kauli ya kisiasa “No Reforms, na wakaitikia No Election” ndani ya ukumbi wa Mahakama mbele ya Hakimu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga ametoa onyo hilo leo June 2, 2025 ambapo pia aliwakumbusha wote wanaohudhuria kesi hiyo kwamba Mahakama ni chombo cha haki kinapaswa kuheshimiwa, na kuwa kitendo cha kuzungumza bila ruhusa ni kosa linalodhoofisha hadhi ya Mahakama.
Akifafanua uamuzi wake hakimu Kiswaga amesema hakuna ubishi kwamba mshitakiwa alitoa maneno ambayo wakili wa utetezi ameyarudia kwa ufasaha akitamka ‘No Reform no election’.
“Hakimu akiingia ndani ya chumba cha Mahakama, Mahakama inakuwa iko kamili tayari kwa kuanza kesi bila kujali nani amekwisha ingia teyari na nani bado”. Amesema Kiswaga
Amesema, Maneno aliyoyasema mshtakiwa tayari mahakama ilikuwa imeshaanza hivyo hilo halikuwa sahihi na si tu kwa mshtakiwa pekee bali hata kwa walioitikia hawakuwa sahihi kwa sababu Mahakama ikishakaa hakuna mtu mwingine wakuzungumza.”
“Natoa onyo si mtu kwa mshtakiwa, lakini hata kwa wengine kutokutamka neno lolote isipokuwa Mahakama, mawakili wa pande zote mnatakiwa kusaidia hili maana nyie ndiyo unaiosaidia Mahakama na siyo sahihi kwamba alichokifanya ni kwa sababu alichelewa kuingia mahakamani,”
Hata hivyo, ametoa muongozo kwa tarehe ijayo kwamba Mahakama itaingia kwanza ndipo kesi iitwe ijulikane ni kesi gani ndipo mshtakiwa aingizwe mahakamani.
Aidha akitoa uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo, Hakimu Kiswaga ameutaka upande wa mashitaka kutoa mrejesho mahakamani hapo juu ya hatua waliyofikia katika upelelezi wa kesi hiyo ili ukamilike, kwani upelelezi kuchukua muda mrefu ni kuchelewesha haki ya mshitakiwa.
Ukirudi kwenye amri ya mwisho Mahakama imesema kwamba kesi iendeshwe kwa kufuata sheria na utaratibu na pia tuache mihemko,” amedai Wakili Katuga
Mapema wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliwasilisha maombi mawili moja wapo ikiwa kuiomba mahakama ichukue hatua dhidi ya kauli hiyo ya Lissu.
kuwa kauli hiyo ya mshtakiwa mbele ya Hakimu ni ishara ya dharau na pia inavunja heshima ya Mahakama ambayo inategemewa itende haki na pia ameomba kuahirishwa kwa kesi hiyo.
“Ombi letu ni Mahakama itoe amri kwa kutumia Kifungu 114 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ili kudhibiti mwenendo wa shauri hili. Mahakama ni chombo cha kutoa haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria, na hivyo lazima iheshimiwe.
Katuga ameongeza kuwa, ukumbi wa Mahakama sio jukwaa la siasa na kudai kwamba Mahakama inaanza ni pale hakimu anapokuwa mahakamani, ambapo ni hatari kama suala hilo lisipoangaliwa itashusha heshima za Mahakama zote .
“Kwa kitendo kilichotokea tunaomba Mahakama itoleee uamuzi, vifungu vya kuzuiwa haya vipo, kwa sababu Mahakama ilisubiri kuita kesi hii hadi hayo haweze kuisha kama hatutaheshemu Mahakama, halafu tunataka itende haki haitakuwa sawa,”amedai
Katika ombi la pili, Wakili Katuga ameomba kuahirisha kesi hiyo kwa sababu upelelezi haujakamilika, jalada limerudishwa ofisi ya upelelezi kumalizia upelelezi baada ya kulisoma na kuona kuna baadhi ya upungufu umeonekana, hawawezi kusema ni kwa eneo gani hilo kwa sababu litaleta mkanganyiko.
Upande wa utetezi wakiongozwa na Wakili Mpare Mpoki amepinga vikali hoja ya kuwa mshtakiwa amekosea. Amedai kuwa Lissu aliingia mahakamani baada ya hakimu, tofauti na utaratibu wa kawaida, jambo lililosababisha mkanganyiko huo. Wakili Peter Kibatala ameongeza kuwa maneno aliyosema Lissu si matusi, na kwa hiyo hayawezi kuchukuliwa kama kosa la jinai.
Wakili Dkt. Rugemeleza Nshalla amedai hakuna jambo la kuchunguzwa zaidi kwani maneno ya Lissu yako wazi, na mshtakiwa anatakiwa kuachiwa huru hadi pale upelelezi utakapokamilika.
Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Kiswaga ameamua kuwa Mahakama haiwezi kufuta kesi kwa sababu upelelezi haujakamilika, lakini akasisitiza kuwa Jamhuri inapaswa kuendelea kutoa mrejesho wa maendeleo ya upelelezi kwa wakati.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 16, 2025 kwa ajili ya kutajwa, huku Mahakama ikisisitiza kuwa heshima na utaratibu wa vikao vya Mahakama lazima uzingatiwe na watu wote wakiwemo mawakili, maofisa wa Mahakama, askari na wananchi.
Katika kesi hiyo inadaiwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam mshtakiwa Lissu akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alitangeneza nia ya kushawishi au kuchochea umma ya kuweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania kwa kusema maneno yafuatayo
“Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko….kwa hiyo tunaenda kukinukisha sana sana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana,”.