Na Silivia Amandius, Bukoba.
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Shilingi milioni 363 kwa vikundi 56 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hatua hii ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuzitaka halmashauri zote kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha makundi hayo kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa wanufaika wa mikopo hiyo, yaliyofanyika tarehe 6 Juni 2025 katika ukumbi wa Chemba, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Bi. Felista Shayo, alieleza masharti muhimu ya mikopo hiyo.
Bi. Shayo aliwataka wanufaika kuhakikisha wanafanya marejesho kupitia namba za malipo walizopewa, ambapo rejesho la kwanza litatakiwa kuanza ndani ya miezi mitatu. Alisisitiza kuwa si ruhusa kubadili aina ya mradi baada ya kupokea fedha na kuwa wanufaika wote wanapaswa kusaini mikataba rasmi ili kuweka mazingira bora ya urejeshaji wa mikopo.
“Serikali inatamani kuona vikundi hivi vikikua na kuwa na tija, kutengeneza ajira, na kuweza kuomba fedha zaidi mara baada ya kumaliza awamu hii, ili kukuza uchumi wao na uchumi wa halmashauri kupitia ulipaji wa kodi,” alisema Bi. Shayo.
Kwa upande wake, Ndugu Amos Samson Igarura kutoka kundi la watu wenye ulemavu aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa fursa hiyo ambayo alisema itamsaidia kujiendeleza kibiashara.
Naye Bi. Josephina Nestory, mwakilishi wa kikundi cha wanawake kutoka Kata ya Katerero, alisema mkopo huo utaongeza mtaji wa kikundi chao na kuwa chachu ya kufikia malengo waliyojiwekea.