Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke,leo ,akitoa hutuba kwa waumini wa Kiislamu (hawapo pichani), baada ya Sala ya Eid El-Adh’ha katika Uwanja wa Nyamagana.
Wauamini wa Kiislamu wasikiliza hotuba baada ya Sala ya Eid El-Adh’ha, leo.
Waumini wa Kiislamu wakiomba dua, leo, baada ya hotuba ya Sala ya Eid El-Adh’ha.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza,Adv. Kiomoni Kibamba, akizungumza na waandishi wa habari, baada ya Sala ya Eid El-Adh’ha.
Mkurugenzi wa Kivulini, Yasin Ali, leo baada ya Sala ya Eid-El Adh’ha, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mmomonyoko wa maadili na kutunza amani kuelekea uchaguzi mkuu.
………..
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke ametoa kwa Watanzania, hususan vijana,kuhakikisha wanadumisha amani,mshikamano na kuhakikisha maadili yanazingatiwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku akitoa angalizo juu ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kauli zinazodhoofisha misingi ya utulivu wa kitaifa.
Akizungumza baada ya Sala ya Eid Al Adha katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza,leo,Sheikh Kabeke amesisitiza umuhimu wa kuendeleza amani,kuheshimu viongozi na kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya.
Amesema Watanzania, hususan vijana, wahakikishe wanadumisha maadili, amani na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 202, huku akitahadharisha juu ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kauli zinazodhoofisha misingi ya amani na utulivu wa kitaifa.
“Kukufuru neema ya amani tuliyonayo, ukikufuru neema ya amani na utulivu Mungu anakuvisha adhabu,anakupamba na njaa ,na tukifikia kukufuru neema ya amani ndugu zangu Waislamu ni kwa sababu tumepoteza maadili.Leo kila mtu sheikh,ni kiongozi haiwezekani,”amesema Sheikh Kabeke.
Amesema mwaka huu tunapoekelea katika Uchuguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani, maadili yaonekane na amani ya nchi ilindwe, kwa sababu Serikali ya Tanzania haina dini lakini watu wake wa dini, asitokee mtu anagombea ubunge ama udiwani akapingwa kwa imani ya dini yake (Uislamu ama Ukristo), hata Rais aliyepo madarakani asipimwe kwa Uislamu wake.
Kwa mujibu wa Sheikh Kabeke Tanzania imekuwa nchi ya kihistoria kwakuongozwa na Marais wa dini zote kwa nyakati tofauti, akianza Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K.Nyerere,aliombewa dua na Waislamu na Wakristo ,akafuatia Ali Hassan Mwinyi(marehemu),Benjamin W.Mkapa,Jakaya Kikwete na John Pombe Magufuli (marehemu) nao waliombewa na waumini wa madhehebu yote,sasa yuko Rais Samia,anastahili kuombewa hima aendelee kuongoza nchi.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema asitokee mtu akampnga Rais kwa sababu ni mwislamu,akamfanyia vituko ,kumwandikia waraka kasha akatoka hadharani kumtukana, hayo si maadili ya nchi yetu.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia uhuru wa kujieleza vibaya kwa kumtukana Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,jambo ambalo halikubaliki kimaadili wala kisheria huku akionya pia dhidi ya tabia ya kuvituhumu vyombo vya dola bila ushahidi wa kutosha kuhusu masuala ya utekaji.
“Kutukana Rais ama wanaye ni kukumtweza na kumkatisha tama ya kuwatumikia wannchi na kuwaletea maaendeleo.Pia, wanaotoa tuhuma wazitoe na suluhisho.Kushutumu pekee haitoshi, wanayo fursa ya kushauri na kusaidia taifa kufikia maridhiano na maendeleo,”amesema
Hata hivyo, Sheikh Kabeke amewaagiza waumini wa kiislamu katika misikiti yote kufunga kwa siku ili kumwombea Rais Dk.Samia na uchaguzi mkuu nchi ivuke salama ambapo alisema watasoma albadir 4444 (Sura Yasin)dhidi ya wanaomwombea mabaya Rais.
Pia,Sheikh Kabeke amewaonya vijana wa Kiislamu wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kupandikiza chuki,migawanyiko ya kidini au kisiasa,wanauchafua Uislamu.
“Uislamu unasisitiza amani, maadili na mshikamano. Haya ndio tunayopaswa kuyaeneza, si matusi wala kejeli.Mitandao ya kijamii si jukwaa la kugawa watu kwa misingi ya dini au siasa. Tuutumie Uislamu kuleta umoja, si migawanyiko,”ameshauri.
Katika kulinganisha hali ya sasa na historia ya baadhi ya mataifa, alitolea mfano wa Libya,ambako machafuko ya kisiasa yaliyoanza kwa maneno na migawanyiko mitandaoni hatimaye yaligeuka kuwa janga kubwa la kitaifa.
Amesema;”Leo hii Walibya wanamkumbuka Hayati Kanali Muammar Gaddafi, lakini ni baada ya kuona machungu ya kuvurugika kwa taifa lao. Tujifunze kutoka kwao.”
Amehimiza wananchi kushiriki uchaguzi kwa amani, kwa kufuata sheria, na kuepuka kuchochewa na propaganda za kugawa umoja wa kitaifa huku akiviasa vyama vya siasa kutenda haki kwa wagombea katika mchakato wa mchujo ikiwemo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutenda haki kwa vyama vyote.