Na Prisca Libaga Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema kuwa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Mkoa wa Arusha ni kuona mkoa huo unakuwa kitovu cha utalii na uchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo, hasa kupitia sekta ya utalii.
Akizungumza wakati wa kikao na viongozi wa mashirika ya reli na bandari waliotembelea Mkoa huo, Mhe. Makonda ameeleza kuwa Rais Samia amedhamiria kwa vitendo kuleta maendeleo Arusha, jambo linalodhihirika kupitia miradi mikubwa inayoendelea kwa sasa, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa na ukumbi mkubwa wa mikutano.
Aidha, Mhe. Makonda amemshukuru Rais Samia kwa kuwatuma viongozi wa Shirika la Reli na Mamlaka ya Bandari kuzungumza na wananchi wa Arusha kuhusu maendeleo yanayokuja mkoani humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Reli Tanzania Ally Karavina ameeleza kuwa wameona umuhimu wa kukagua reli ya kutoka Arusha hadi Dar es Salaam, na kufikiria namna ya kuunganisha njia hiyo hadi Tanga na tayari wamepata mradi wa ukarabati wa reli hiyo ili kuongeza kasi ya usafiri wa treni kufikia wastani wa kilomita 70 kwa saa.
“Yanayokuja Arusha yanaridhisha. Mpango wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR bado upo kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na reli hiyo itarahisisha usafirishaji wa magadi soda kutoka Engaruka hadi kufika Musoma,” amesisitiza Karavina.
Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA) Plusduce Mbosaa ametoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, kuchangamkia fursa ya ujenzi wa Bandari Kavu jijini Arusha na kuongeza kuwa wako tayari kutoa vibali kwa mtu au taasisi yoyote yenye nia ya kuwekeza kwenye mradi huo.
Aidha, mizigo yote itakayopokelewa kupitia bandari ya Arusha itapitia katika bandari kavu hiyo, hatua itakayorahisisha shughuli za usafirishaji na kuongeza ufanisi katika biashara.

