Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasisitiza Watanzania waishio nchini China (Dispora) kuchangamkia fursa ikiwa ni pamoja na kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nchini humo.
Hayo yamejiri wakati Mheshimiwa Kombo alipozungumza na Watanzania hao katika mji wa Guangzhou jimbo la Guangdong tarehe 15 Juni, 2025 ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi inayoendelea nchini China.
Mhe. Kombo alisema kuwa bidhaa za Tanzania zimepewa upendeleo maalum kupitia ushirikiano wa kimkakati uliopo kati ya Tanzania na China na hivyo bidhaa zote kutoka nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zimeruhusiwa kuingia nchini China bila ushuru wa forodha.
‘’Chukueni hatua kwa kuchangamkia fursa hiyo na muendelee kuwahamasisha Watanzania kuingiza bidhaa kwa wingi China ili kuleta urari wa biashara kati yetu,’’ alisisitiza Mhe. Kombo.
Kadhalika, aliwahamasisha kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuleta wawekezaji wenye sifa, hatua itakayosaidia kuongeza ajira na kukuza shughuli za uchumi nchini.
Hii inaweza kufanyika kupitia ushirikiano wa ubia baina ya Wachina na Watanzania ili kukidhi vigezo vya uwekezaji kwa baadhi ya sekta zenye kigezo hicho.
Vilevile, amewaasa kufuata sheria na taratibu za China na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuchafua taswira nzuri ya nchi yao na kwamba waendelee kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania nchini China.
Naye, Mwenyekiti wa Watanzania waishio katika jimbo la Guangdong, Bw. Hashim Twalib Shelali ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapa ushirikiano Watanzania kupitia ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo Beijing, pamoja na Ofisi ndogo ya Ubalozi iliyopo Guangzhou.
Pia, ameeleza kuwa wataendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kukuza kipato chao na cha taifa kwa ujumla pamoja na kushiriki katika kushughuli za maamuzi ikiwemo kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaofanyika mwezi Oktoba, 2025.
Wakati huo huo Waziri Kombo alifanya mazungumzo na watumishi wa Ubalozi Mdogo wa Tanzania mjini Guangzhou ambapo alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa kutekeleza majukumu yao ya uwakilishi na kutekeleza diplomasia ya uchumi inayopewa msisitizo na Sera ya Mambo ya Sera iliyofanyiwa maboresho na kuzinduliwa tarehe 19 Mei, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aliwaeleza watumishi hao kuwa wapo katika nchi ya kimkakati kwa ushirikiano na Tanzania katika eneo la biashara na uwekezaji ambavyo ni msingi katika kuleta mageuzi ya kiuchumi.