Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Mwema Punzi (kulia) akitoa ufafunuzi wa utendaji wa ofisi hiyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyofanyika leo, Juni 16, 2025, katika Viwanja vya Mbagala Maturubai, jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mkuu wa Kituo cha Msaada wa Sheria Wilaya ya Temeke Wakili Fortunata Shija (kushoto) akipokea zawadi baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyofanyika leo, Juni 16, 2025, katika Viwanja vya Mbagala Maturubai, Dar es Salaam.
Wakazi wa Mkao wa Dar es Salaam wakiwa katika banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakipatiwa huduma ya msaada wa Kisheria.
Wadau mbalimbali wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyofanyika leo, Juni 16, 2025, katika Viwanja vya Mbagala Maturubai, Dar es Salaam
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga kikamilifu kutoa msaada wa kisheria bila malipo kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, iliyozinduliwa leo, Juni 16, 2025, na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika Viwanja vya Mbagala Maturubai, jijini Dar es Salaam.
Kampeni hiyo ya utoaji wa huduma za kisheria bure itadumu kwa muda wa siku nane kuanzia leo, ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria, kutatua migogoro, pamoja na kuwasaidia kupata haki zao.
Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dar es Salaam, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Mwema Punzi, amesema kuwa timu ya wataalamu wa sheria imeweka kambi katika Viwanja vya Maturubai Mbagala, ili kuhakikisha wananchi wote wanaofika kwenye banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanapatiwa huduma kwa haraka na kwa ufanisi.
Wakili Punzi amesema huduma zinazotolewa zinahusiana na masuala mbalimbali ya kisheria, hususan yale yanayohitaji utaratibu maalum wa kisheria ili kupata ufumbuzi.
“Mwananchi yeyote anayehitaji msaada wa kisheria anakaribishwa katika banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata huduma hiyo kuhusu masuala mbalimbali yanayomkabili, yakiwemo ardhi na hifadhi,” amesema Wakili Punzi.
Aidha, ameongeza kuwa mwitikio wa wananchi ni mkubwa, kwani wengi wamejiandikisha tayari kwa ajili ya kupata huduma hiyo ya kisheria katika banda hilo.
Wakili Punzi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Mbagala Maturubai ili kupata elimu ya kisheria na kuhakikisha kuwa haki zao zinapatikana ipasavyo.
Kwa upande wao wananchi waliofika katika banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiwemo Emmanuel John pamoja Asha Rajabu wameishukuru ofisi ya wanasheria mkuu kwa kuwapatia msaada wa kisheria kwani unakwenda kuwa msaada katika kuhakikisha haki zao zinapatikana.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imebeba kauli mbiu inayosema : Msaada wa kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo.