Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha utumishi wa umma kwa kutumia teknolojia, ubunifu na kuboresha huduma kwa wananchi.
Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo, Juni 17, 2025, wakati akizindua Kongamano la Kitaaluma la Utumishi wa Umma lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), katika hoteli ya Verde, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akihutubia washiriki wa kongamano hilo, Rais Mwinyi alisema kuwa utumishi wa umma ni uti wa mgongo wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kwamba mafanikio ya taifa lolote yanategemea ubora wa huduma zinazotolewa katika sekta hiyo.
Alisisitiza kuwa kaulimbiu ya kongamano hilo isemayo “Mchango wa Uongozi, Teknolojia na Ubunifu katika Kufikia Tanzania Tuitakayo” inapaswa kuwa msingi wa mijadala na mabadiliko katika taasisi za umma.
Aidha, Rais Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mifumo ya kidijitali inaimarishwa ili kuongeza uwazi, kuondoa urasimu na kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tunahitaji utumishi wa umma wenye maadili, uwajibikaji na uwezo wa kutumia teknolojia kisasa ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi,” alisema Dkt. Mwinyi.
Katika hotuba hiyo, Rais Mwinyi pia alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake katika kuimarisha mshikamano wa Muungano na kuendeleza ushirikiano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Ragey Mohamed, aliwataka washiriki wa kongamano hilo kuhakikisha kuwa maazimio yatakayopitishwa yanatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya umma na maendeleo ya taifa kwa ujumla.