Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa akizungumza wakati akifunga Kongamano la 13 la Kisayansi la MUHAS lililofanyika 19 Juni, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mwenyekiti wa Kongamano Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Raphael Z. Sangeda, akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la 13 la Kisayansi la MUHAS lililofanyika 19 Juni, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila.
Kaimu Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo MUHAS, Idara ya Tafiti na Ushauri wa Kiutaalamu Prof. Bruno Sunguya akizungumza jambo wakati wa kufunga Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
Mwanafunzi kutoka Shule ya Afya na Mazingira MUHAS, Bi. Bhoke Juma akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa akitoa zawadi kwa watafiti waliowasilisha Mawasilisho mazuri ya utafiti katika Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Cha MUHAS.
…………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Watafiti sekta ya afya wamefanikiwa kuwasilisha tafiti zaidi ya 200 katika Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ambazo zimejikita kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali zikiwemo matumizi ya dawa, mifumo ya afya pamoja na matumizi ya teknolojia.
Akizungumza leo Juni 19, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga kongamano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa amesema kuwa lengo kuu la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau wa utafiti ili kuwasilisha matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa na chuo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Prof. Kamuhabwa amesema kuwa katika kongamano hilo kulikuwa na mawasilisho mbalimbali ya tafiti, ambapo tafiti nyingi za MUHAS zimejikita katika kutafuta suluhisho la matatizo yanayohusiana na matumizi ya dawa na mifumo ya afya ili kuisaidia jamii na taifa kwa ujumla.
“Kongamano hili la kisayansi la mwaka huu limebaini mambo mengi ya msingi, ikiwemo mifumo ya afya na namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali kama milipuko ya magonjwa na majanga ya asili. Swali la msingi ni: tumejiandaaje?” amesema Prof. Kamuhabwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Prof. Raphael Z. Sangeda, amesema kuwa baada ya kongamano hilo, kutafanyika maazimio mahsusi yatakayofanyiwa kazi ili kuleta matokeo chanya kwa taifa.
Ameeleza kuwa tafiti 200 zilizowasilishwa zina mchango mkubwa kwa jamii, kwani zinalenga kusaidia wananchi kutatua changamoto zilizopo na kufanikisha malengo ya serikali katika sekta ya afya.
Washiriki wa kongamano hilo, akiwemo mwanafunzi kutoka Shule ya Afya na Mazingira ya MUHAS, Bi. Bhoke Juma, wameishukuru MUHAS kwa kuandaa kongamano hilo, huku wakisema kuwa limekuwa na manufaa makubwa kwao binafsi na kwa taifa kwa ujumla.
Kongamano hilo ambalo limehudhuriwa na zaidi ya washiriki 500, lilikuwa na kaulimbiu isemayo:
“Kubadili Mifumo ya Afya Afrika: Kuweka Kipaumbele katika Bunifu na Tafiti katika Kukabiliana na Changamoto Nyumbufu za Afya Duniani.”
Kaulimbiu hiyo ilichaguliwa kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya kwa kutumia ushahidi wa kisayansi, teknolojia bunifu, na ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kukabiliana na changamoto mpya na endelevu kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya tabianchi, na ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.