Naibu Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania Steria Ndaga, ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini amewataka watumishi wa TANAPA kuongeza juhudi katika kufanya kazi hasa katika msimu huu mpya wa utalii ambao umeanza mwezi juni ili kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa kikamilifu.
Ameyasema hayo jana juni 19, 2025 katika kikao cha Menejimenti Kuu ya Kanda ya Kaskazini kikijumuisha Wakuu wa Hifadhi, Wakuu wa Vitengo vya Uhasibu na Utalii pamoja na Wakuu wa Vitengo Makao Makuu ya Kanda ya Kaskazini, kikao ambacho kililenga kupitia na kujadili taarifa za utendaji kazi katika kipindi cha miezi 11 iliyopita.
Aidha Kamishna Ndaga alisema, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na shirika ni muhimu kuhakikisha mapato yanakusanywa kikamilifu huku watumishi wakiendelea kujenga utamaduni wa mahusiano mazuri mahali pa kazi na kuweka mazingira rafiki ya utendaji kazi wenye tija.
Pamoja na hayo, Kamishna Ndaga aliwahimiza watumishi wa shirika kuendelea kutoa taarifa muhimu kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi. Alisisitiza kwamba utoaji wa taarifa kwa wakati si tu unarahisisha ufanyaji wa maamuzi, bali pia unachangia moja kwa moja katika kufanikisha malengo mahususi ya shirika.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania linasimamia jumla ya hifadhi 21 zilizogawanyika katika kanda nne ikiwemo Kanda ya Kaskazini ambayo inasimamia jumla ya hifadhi tano ambazo ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Tarangire, Ziwa Manyara,Arusha,Kilimanjaro pamoja na Mkomazi.