Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mhe. Rosemary Senyamule leo tarehe 23/06/205 amezindua kontena mbili za kikundi cha Wanawake na Samia na Watu wenye Ulemavu wa Ngozi (FDH) Dodoma ikiwa na utekelezaji wa ahadi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),Dkt. Venance Mwasse ya kuwainua kiuchumi makundi haya maalum.
Amempongeza Dkt. Mwasse kwa kufanyia kazi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi na salama Afrika na duniani kote
Akizungumza katika mkutano huo,Mkuu wa Mkoa amebainisha kuwa Dkt. Mwasse amekuwa mwepesi sana wa kuyatafsiri maono ya Mhe.Rais na kuyatekeleza kwa haraka.
Amesema kuwa moja ya mambo ambayo ameyatafsiri kwa vitendo maono ya Rais Samia ni pamoja na kuyasaidia makundi maalum na hasa kuwapatia fursa za kiuchumi na pia uhifadhi wa mazingira kupitia usambazaji wa nishati ya Rafiki Briquettes
“STAMICO kupitia MD wake. wamefanya jambo kubwa kuwawezesha makundi haya maalum kupitia kazi hii mmewakomboa kiuchumi na pia kuunga mkono juuhudi za Mhe.Rais za kuhifadhi mazingira”,amesema.
Ametoa shime kwa vijana na watu wenye mahitaji maalumu kutumia fursa ambazo zinapatikana katika mnyororo wa biashara ya Rafiki Briquettes ambapo itawasaidia kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO amesisitiza dhamira ya Shirika ya kuwawezesha Wanawake na Samia nchi nzima na kuwa ajenda ya milele ili kuhakikisha wananufaika na ubunifu wa Shirika katika bidhaa ya Rafiki Briquettes.
Ametoa rai kwa Wanawake na Samia nchi nzima kutumia fursa hii katika utekelezaji wa miradi hii ili iwaletee tija katika maisha yao.
Awali katika risala zao,Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa Vikundi vya Wanawake na Samia nchini kote, Bi Fatuma Madidi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Disabilities Hope (FDH), Bw Michael Salali wametoa pongezi za dhati kwa Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO kwa juhudi kubwa anazo zifanya za kuwawezesha kushiriki katika mnyororo wa Biashara ya Rafiki Briquettes hivyo kunufaika na rasilimali za Taifa.