Na Alex Sonna, Dodoma
Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imetumia vyema fursa ya ushiriki wake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo kongwe ya habari nchini.
Akizungumza kwenye kilele cha maonesho hayo yanayofanyika jijini Dodoma, Afisa Uhusiano wa TSN, Nadhifa Omary, amesema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa taasisi yao kukutana moja kwa moja na wananchi, kusikiliza maoni yao na kuwapa uelewa wa karibu kuhusu majukumu ya TSN katika sekta ya habari na uchapishaji.
“Katika maonesho haya tumekutana na Watanzania wengi kutoka sehemu mbalimbali,tumetumia nafasi hii kuwaelimisha juu ya namna ofisi yetu inavyofanya kazi, huduma tunazotoa na mchango wa TSN katika kuhifadhi kumbukumbu muhimu za kitaifa,” amesema Nadhifa.
Ameongeza kuwa TSN, mbali na kuchapisha magazeti ya HabariLEO na Daily News, pia inajihusisha na uchapishaji wa machapisho mbalimbali kama kalenda, diary, vitabu, na nyaraka nyingine muhimu kwa matumizi ya taasisi za umma na binafsi.
Aidha, amebainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamekuja na kaulimbiu yenye lengo la kuhimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na uwajibikaji katika utumishi wa umma, jambo ambalo TSN imelipa uzito kwa kuendelea kujiimarisha kiteknolojia.
“Serikali imeendelea kuboresha utendaji wetu kwa kutupatia mtambo mpya wa kisasa, unaotuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kwa kasi inayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia,” amefafanua.
Aidha ametoa wito kwa Taasisi ambazo bado hazina mifumo imara ya kuhifadhi kumbukumbu kushirikiana na TSN kwa lengo la kuhakikisha historia na taarifa muhimu za taifa zinatunzwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


