Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile wakati akizungumza na maafisa usafirishaji
Mganga mkuu wa manispaa ya Sumbawanga wakati akizungumza na maafisa usafirishaji walioandaa kampeni hiyo
Mwenyekiti wa chama cha bodaboda mkoa wa Rukwa akielezea namna walivyoandaa kampeni ya uchangiaji wa damu
Maafisa usafirishaji manispaa ya Sumbawanga.
Picha na Neema Mtuka
…………..
Na, Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Maafisa usafirishaji wilayani Sumbawanga, wakiwemo waendesha bodaboda, wametakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani pamoja na kulinda vyombo vyao na maisha yao, kwa kuwa wao ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya taifa.
Wito huo umetolewa leo June 25,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uchangiaji damu iliyoandaliwa na chama cha maafisa usafirishaji mkoa wa Rukwa.
Chirukile amesema kuwa ni vyema maafisa hao wakazingatia sheria za usalama barabarani na kuachana na matumizi ya vilevi pindi wanapoendesha vyombo vya moto.
“Ukiwa barabarani hakikisha unazingatia sheria ili kujilinda wewe na watumiaji wengine wa barabara bila kusahau kuvaa helmeti kwa kuwa barabarani unaweza wewe kuwa makini lakini mwenzako akakusababishia ajali hivyo ni vyema kuzingatia hayo.”amesema Chirukile
Akizungumzia kuhusu kujitoa kwao na kuandaa kampeni ya uchangiaji wa damu amewapongeza kwa zoezi hilo la kiutu ambalo linakwenda kupunguza changamoto ya mahitaji ya damu kwa wagonjwa wenye uhitaji na jambo hilo limechochea upendo.
“Ninawapongeza sana kwa kuandaa kampeni hii hata mbele ya mwenyezi Mungu tayari umepokea thawabu kwa kufanya jambo la kibinadamu la uchangiaji wa damu nina matumaini baada ya miezi mitatu mtarudi tena na kuchangia damu .”Amefafanua Chirukile.
Katika hotuba yake, Chirukile amewataka maafisa hao wa usafirishaji kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wao katika maendeleo ya taifa kupitia mifumo ya kidemokrasia.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga Robert Rwebangira Mganga amesema Halmashauri hiyo inawategemea kwa kiasi kikubwa waendesha bodaboda kutokana na mchango wao mkubwa katika kutoa huduma kwa jamii, hasa katika usafirishaji wa wagonjwa na wahitaji wengine wa dharura.
Amesema wapo wagonjwa ambao wanahitaji damu kwa dharura wakiwemo akina mama waliojifungua na kupoteza damu nyingi ,majeruhi wa ajali na wagonjwa wenye matatizo ya kuishiwa damu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha bodaboda mkoa wa Rukwa Leonard Milambo amesema kuwa wameamua kuigusa jamii katika upande wa uchangiaji wa damu na kutaka vyana vingine vijitokeze katika kushiriki mambo ya kijamii.
Amesema kutokana na watu wengi kupoteza maisha kutokana na kukosa damu ndio jambo liliko wasukuma kuandaa kampeni hiyo.
Alfred Njeza ambaye ni afisa usafirishaji kutoka katika kata ya Mazwi amesema lengo lao hasa ni kuhakikisha wanaigusa jamii moja kwa moja kwa kushiriki katika uchangiaji wa damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wa dharura wanaohitaji damu kwa haraka .
“Si tu katika kusafirisha abiria bali tunatamani kuona tunaigusa jamii kwa kadiri ya uwezo wetu na ndio maana tuliona tunaweza kuwa na kamepni hiii ya uchangiaji wa damu na tukaigusa jamii kwa kiwango kikubwa .”amesema Njeza.
Aidha, maafisa usafirishaji walioshiriki katika tukio hilo wamesema kampeni hiyo ni uthibitisho wa namna wanavyomuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kuboresha huduma mbalimbali nchini, ikiwemo sekta ya afya.