NA DENIS MLOWE IRINGA
MWENYEKITI Mstaafu wa Ccm Wilaya ya Kilolo 2017-2022 Kilian Edson Myenzi ametangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Kilolo huku akiweka vipaumbele mbalimbali endapo atachaguliwa na Chama cha Mapinduzi atakwenda kuwasemea.
Akiongea na waandishi wa habari kabla ya kuchukua fomu amesema pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya awamu ya Sita Kilolo inahitaji Kiongozi anayeweza kuwaunganisha Wanakilolo wote ,kuwa sauti kwa wasioo na sauti na kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayoletwa na serikali.
Alisema kuwa wilaya Kilolo inahitaji kijana mchapakazi na mwenye uadilifu mkubwa ikiwemo kuwasimamia wakandarasi kwenye miundombinu ya barabara ili barabara ziweze kupitika kwa misimu yote ya Masika na kiangazi.
Akizungumza kwa uchungu alisema kuwa Kilolo ni wilaya yenye Utajiri mkubwa wa Rasilimali Watu,ardhi, misitu, madini,mazao lakini bado barabara ni mbovu hazipitiki hali inayoathiri ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Kilolo.
Alisema kuwa endapo atapata ridhaa utakuwa ni mwisho wa barabara kutopitika mwaka mzima kwani anao muarobaini wa kutibu tatizo hilo kwenye miundo mbinu ya barabara.
Ameenda Mbele zaidi kwa kudai kuwa ataishauri serikali kujenga barabara za zege maeneo korofi ili kupunguza gharama na kuifanya Kilolo kuwe eneo la kuzalisha Dhahabu ya kijani kama parachichi na mazao ya mbogamboga.
Aidha aliongeza kuwa moja ya ndoto ni kuhakikisha barabara ya kutoka Ipogoro Mdete hadi Mgeta inakamilika endapo watampa ridhaa ya kuwa Mbunge jimbo hilo kuweza kupitika kwa mwaka mzima.
Amehitimisha kwa kusema Dhamira ya Mheshimiwa Raisi Daktari Samia Suruhu Hassan Itafikiwa kwa kupata Wasaidizi vijana Wenye Maono kwa kauli mbiu yake isemayo *Ni Wakati wa Mabadiliko Kiliani anatosha*