:::::::
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Katika hatua kubwa ya kuleta mapinduzi ya
kiuchumi na kuchochea ukuaji wa biashara bunifu nchini, Mradi wa Ubunifu wa
FUNGUO umetangaza fursa mbili mpya za ufadhili zenye thamani ya zaidi ya
Shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya kusaidia wajasiriamali wa Tanzania – hususan
wale wanaoendesha biashara endelevu kwa mazingira.
Fursa hiyo imetolewa jijini Dar es
Salaam Juni 27, 2025, na kuambatana na wito maalum kwa vijana na wanawake
nchini kuhakikisha wanachangamkia fursa hizo ambazo zimeelezwa kuwa za aina
yake katika kuchochea ajira, ubunifu na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati
wa uzinduzi wa fursa hizo, Karina Dzialowska, Mkuu wa Idara ya Uchumi na
Utawala wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, amesema kuwa FUNGUO limekuwa
daraja la matumaini kwa wajasiriamali wachanga na wadogo kote nchini.
“Kilichoanza kama mradi wa majaribio miaka
minne iliyopita, sasa ni mhimili wa mfumo wa Tanzania wa kusaidia biashara
changa. FUNGUO si tu linatoa fedha, bali linajenga uwezo na kuwaunganisha
vijana na wanawake na masoko ya ndani na nje,” alisema Dzialowska huku
akisisitiza kuwa asilimia 40 ya ruzuku hizo zimekusudiwa kwa wanawake.
Aidha, alitoa wito mahsusi kwa wanawake na
vijana walioko mijini na vijijini kuwa na uthubutu wa kuwasilisha maombi ya
ufadhili huo, akisisitiza kuwa hakuna ndoto ndogo iwapo kuna mpango madhubuti
na dhamira ya kweli.
Kwa upande wake, William Nambiza, Mratibu
wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Finland nchini, alieleza kuwa
kupitia mpango maalum wa #GreenCatalyst, serikali ya Finland inalenga kuchochea
ubunifu wa ndani katika sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira.
“Tunahitaji ajira ambazo si tu zinaongeza
kipato, bali pia zinalinda mazingira yetu. Biashara zinazojikita katika
matumizi bora ya rasilimali na kuongeza thamani ya mazao ya misitu zinahitaji
kupewa msukumo mpya,” alisema Nambiza, akiwasihi wajasiriamali wengi zaidi
kuwasilisha maombi kupitia dirisha la mpango huo.
Naye John Rutere, Naibu Mwakilishi Mkaazi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania), alisisitiza kuwa
FUNGUO si mradi wa kawaida, bali ni “safari ya kujenga kizazi cha biashara
zinazotatua changamoto halisi.”
“Tunaangalia mbali zaidi ya faida binafsi.
Tunataka kuona biashara zinazobadili maisha ya watu, zinazoajiri, na
zinazolinda mazingira yetu. Hadi sasa, ajira zaidi ya 5,000 zimezalishwa
kupitia FUNGUO, na zaidi ya TZS bilioni 15 zimekusanywa kama uwekezaji wa
nyongeza kutokana na mitaji tuliyowekeza,” alisema Rutere.
Mradi wa FUNGUO unatekelezwa na UNDP kwa
ushirikiano na Umoja wa Ulaya, Finland na Uingereza (kupitia FCDO), ukilenga
kusaidia biashara ndogo, ndogo sana na za kati (MSMEs) katika sekta mbalimbali.
Fursa hizi mpya ni sehemu ya azma ya
kujenga uchumi jumuishi unaojali mazingira, ubunifu na usawa wa kijinsia.
Dirisha la maombi kwa ufadhili huo lipo wazi, na wajasiriamali kutoka mikoa
yote ya Tanzania wanakaribishwa kuwasilisha maombi yao kupitia tovuti rasmi ya
FUNGUO.