Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ametuma salamu za pole kwa familia zote zilizoguswa na msiba huu uliosababishwa na ajali ya magari mawili kugongana na kuwaka moto.
Aidha, Mhe. Kasilda anaufahamisha umma kuwa miili mitano, ikiwemo ya wanawake wanne na mwanamume mmoja, iliyohifadhiwa kwenye hospitali ya Mji Same, Serikali tayari imeruhusu ichukuliwe na kuendelea na taratibu za mazishi.
Kwa wale ambao hawajafanikiwa kuona miili ya ndugu zao, Serikali ya wilaya imewaomba kwenda KCMC wakiwa na familia zao (baba, mama na watoto) kwa ajili ya kipimo cha vinasaba (DNA) ili kubaini miili ya ndugu zao na kuichukua kwa mazishi kwa taratibu za kifamilia, kwani miili hiyo iliharibika vibaya kutokana na moto huo.
Ndugu ambao tayari vinasaba vimeshachukuliwa kwa ajili ya kubaini ndugu zao, siku ya Alhamisi tarehe 3/7/2025, Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro itawakabidhi miili itakayobainika kwa taratibu za mazishi na zoezi la kuchukua sampuli za DNA linaendelea.
Vilevile, Mhe. Kasilda ametuma pole kwa watu wote na kuwaomba wananchi wa Wilaya ya Same kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu ambacho Serikali pamoja na wananchi wake wanapitia, kwa kuondokewa na wananchi wengi wa Mji wa Same.