Mkuu wa Mkoa wa Dar es alaam Mhe Albert Chalamila amewataka wenyeviti wa Serikali za mitaa pamoja na watendaji wa Kata Mitaa Mkoani humo kusimamia ulinzi na usalama kwenye ngazi ya mitaa na kata ili kuhakikisha Mkoa huo unakua Salama bila uwepo wa matukio ya uvunjifu wa amani wakati wote.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na Wenyeviti, Watendaji wa Kata na mitaa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Diamomd Jubilee RC Chalamila amesema suala la ulinzi na usalama linapaswa kuanzia kwenye ngazi ya mitaa na kata hivyo amewataka viongozi hao wa mitaa kusimamia suala hilo kwani katika baadhi ya mitaa kumekua na matukio ya uvunjifu wa amani.
RC Chalamila amewataka viongozi hao ngazi ya Mitaa na Kata kusaidia kutatua changamoto za wananchi na sio wao kuwa ni chanzo cha kuongeza changamoto kwa wananchi ambapo pia ametumia nafasi hiyo kuwataka wenyeviti na watendaji kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo waendelee kuhimiza wananchi kuanzia ngazi ya mtaa kushiriki uchaguzi
Aidha RC Chalamila kupitia Kikao kazi hicho amewataka wenyeviti wa mitaa pamoja na watendaji wa mitaa na Kata kuhamasisha wananchi na wafanyabiashara kulipa kodi ili kuwezesha Serikali kuwa na fedha za kutosha ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, kwani Rais Dkt Samia anahitaji fedha ili kuendelea kuleta maendeleo kwa masilahi mapana ya umma.
Aidha ameongeza kuwa katika hotuba ya Rais wakati akiapisha viongozi hivi karibuni Mkoani Dodoma aliwasisitiza wakuu wa mikoa mambo manne ikiwemo umuhimu wa kulinda amani, kukusanya mapato kusimamia miradi ya maendeleo pamoja na kushuka kwa wananchi kusikiliza kero zao hivyo ili kutimiza hayo viongazi ngazi ya mitaa na kata wana nafasi kubwa
Kwa upande wake Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es salaam SACP Jumanne Muliro amesema ni muhimu kwa wenyeviti wa mitaa pamoja na watendaji wa mitaa na Kata kushirikiana na jeshi la polisi kuimarisha amani kuanzia ngazi ya mitaa hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu na mwezi Octoba 2025.