NA DENIS MLOWE IRINGA
MKURUGENZI wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Sylvester Mwakitalu amewataka Waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwenda kuitumia vizuri nafasi waliyopata katika Utumishi wa Umma na kuhakikisha wanashinda kwa asilimia 85 makosa yote ya jinai ambayo watafungua nchini.
Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Sheria na Katiba Dr. Damas Ndumbaro , wakati wa ufungaji wa mafunzo maalum kwa watumishi hao wapya Mkurugenzi wa Mashtaka, Sylvester Mwakitalu alisema kuwa katika kufanikisha ushindi wa kwa asilimia hizo lazima kazi ifanyike kwa weledi, uadilifu na kuzingatia haki.
Alisema kuwa majukumu waliyopewa na serikali ni majukumu nyeti sana na usipoyatekekeleza kwa uaminifu amani ya nchi itakuwa katika hatari.
Mwakitalu aliongeza kuwa suala la weledi, uadilifu uaminifu kwa watumishi ndio msingi mkubwa wa kutenda haki kwa wananchi ambao watuhumiwa katika makosa ya jinai .
Aliongeza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni muhimili muhimu wa utekelezaji wa haki na ulinzi wa maslahi ya umma kupitia mashauri ya jinai kwa maana hiyo mkienda kazini hakikisheni mnafanya kuchagua mpelelezi mzuri wa makosa na unaifungua kesi ukiwa na upelelezi wa kutosha ili haki itendeke.
Mwakitalu aliongeza kuwa hivi karibuni wanatarajia kuwa ofisi katika kila wilaya hapa nchini hivyo hawatarajii mtumishi kuchagua eneo la kazi, kuleta samahani zozote.
Aliwataka pia wawe na tayari wakati wowote na kufanya kazi zaidi ya muda wa kazi, kwani kuna nyakati watumishi wengine watakuwa likizo na wengine wanafanya kazi.
Aidha aliwataka watumishi kutunza mali za ofisi na kutoa onyo kwa madereva wa ofisi hiyo kuzingatia sheria na kutunza magari ya ofisi
Baadhi ya waliopata mafunzo hayo Novatus Mulungu ambaye ni dereva alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa waajiriwa wapya hivyo watayazingatia kwa kiasi kikubwa.
Mafunzo hayo yamejumuisha jumla ya washiriki 148 ambapo kuna Makatibu Sheria 20, Mawakili wa Serikali 102, Madereva 24, Muhasibu 01 na Msaidizi wa Maktaba 01.




