Na Sophia Kingimali.
WIZARA ya Katiba na Sheria imetoa rai kwa wananchi kutembelea banda la Katiba na Sheria ili kupata elimu inayohusu masala ya Sheria lakini pia kupata msaada wa kisheria kwa wenye matatizo mbalimbali yanayohitaji msaada.
Pia wizara hiyo imeibuka mshindi wa kwanza kundi la Wizara zote zilizoshiriki maonesho ya 49 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2025 .
Sagini ametoa wito huo leo julai 8,2025 alipotembelea maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara Sabasaba yanaendelea katika viwanja vya Mwàlimu Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia na waandishi wa habari kwenye Banda hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema wanastahili kuwa washindi wa kwanza kwani wananchi wameridhishwa na utolewaji wa huduma.
“Niwapongeze wataalamu Wetu, mawakili wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria niwapongeze Waziri na Katibu Mkuu kukubali kuleta Idara zote za Katiba na Sheria hapa ambao pia hutoa Elimu ya masala mbalimbali ya yanayoratibiwa na hizo Idara,”amesema.
Akizungumzia kampeni ya Msaada wa kisheria, Sagini amesema huduma hiyo imeleta matokeo chanya ambapo serikali imeridhishwa na utolewaji wa huduma hiyo.
“Wizara ya Katiba na Sheria inalifanya jambo hili kuwa endelevu kwa kupeleka maafisa ngazi ya Halmashauri ambapo wanawasaidia wananchi kwa kushirikiana na taasisi zingine za kisheria,”alisema.
Aidha Ameongeza kuwa wameweka kipaumbele kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sekta kama Ardhi ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.
Amefafanua kuwa licha ya migogoro ya Ardhi,pia kuna migogoro ya ndoa ambapo Elimu inatakiwa kutolewa kwa kushirikiana na maafisa walipo kwenye Mamlaka ngazi za Mitaa na wataalamu wa msaada wa kisheria waliopo ambao ni wadau wa huduma za msaada wa kisheria kwa kuelimisha wananchi kuhusu ndoa.
Akiwa kwenye maonesho hayo alitembelea Banda la Mahakama, Wakala wa Vizazi na Vifo(RITA) ambapo amebaini ushiriki wa watu wengi waliojitokeza kuomba vyeti vya kuzaliwa.
Amesema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa huduma ya utoaji wa vyeti upo hadi ngazi za Wilaya hivyo hakuna sababu ya kusubiri wakati wa maonesho ya Sabasaba ambapo wengine hukutwa vyeti vyao vimeshapelekwa kwenye Wilaya wanapotoka.