NA DENIS MLOWE IRINGA
MENEJA mkuu wa Kampuni ya Zana Bora Limited Hassan Athuman Hassan amewataka wakulima kuachana na kilimo cha mazoea kwa kutumia zana duni za kilimo katika uzalishaji na kujikita katika matumizi ya zana za kisasa ili kuweza kuzalisha mazao mengi zaidi.
Wito umekuja baada ya kampuni hiyo kuwajengea uwezo wakulima kwa kuwafikishia zana za kilimo karibu kabisa na mashamba yao ili iwe rahisi katika kununua zana hizo tofauti na awali.
Akizungumza na waandishi wa habari. Meneja Hassan alisema kuwa kampuni ya Zana Bora Limited imekuja kuwa mkombozi wa wakulima Nyanda za Juu Kusini hiyo baada ya kutoridhishwa na mavuno yanayopatikana kila mwaka kwa wakulima licha ya kuwa mikoa hiyo ina maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali.
Alisema kuwa kilimo cha mkono kimepitwa na wakati na endapo mkulima anahitaji kuongeza mazao inabidi awe na shamba lenye ekari nyingi hivyo umuhimu wa kutumia Zana za Kisasa unahitajika kwa kiasi kikubwa na Zana hizo zinapatikana Zana Bora Limited.
“Ni vyema wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nawasisitiza matumizi ya zana bora za kilimo ili kupanua wigo wa uzalishaji wenye kuleta tija kwa wakulima hao na hata viwanda na uchumi kwa ujumla” Alisema
Alisema kuwa wao kama Zana Bora Limited wameingia ubia na benki kwa ajili ya wakulima kwenda kukopa benki na kisha kuja kununua Zana za Kisasa hivyo kutumia fursa ya kukopa kutoka kwenye taasisi za kifedha kama vile NMB , Azania ambao wanakubaliana na kisha waweze kununua matrekta na hata pembejeo zinginezo.
Naye wakala Mkuu wa kampuni ya Zana bora Limited wa Kanda Nyanda za Juu Kusini ,Job Mdeluka alisema kuwa kwa sasa wameleta zana bora kwa ajili ya wakulima hivyo ni wakati wao kuchangamkia fursa hizo ili wakue katika ukulima kuliko kuendelea na kilimo cha zamani.
“Wakulima wanatakiwa kuacha kutumia jembe la mkono na kujikita katika matumizi ya matrekta ili kulima maeneo makubwa kwa wakati na kupata matokeo ridhishi na kupunguza upotevu mkubwa wa chakula” alisema
Alisema kuwa wakulima waliobadilika na kutumia Zana za Kisasa wamekuwa na mafanikio makubwa na hii imejionyesha kwa baadhi yao kubadilika na kuanza kuagiza Zana bora ambapo hadi sasa wana oda ya Kubota power 100 baada ya kuona mafanikio ya wale wanaotumia zana hiyo.
Alisema kuwa wamekuwa wakihamasisha matumizi ya zana bora za killmo ikiwa ni pamoja kujenga uwezo wa zana za kilimo na kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa zana wanazotumia katika shughuli zao za kilimo ili kufkkia dhamira ya Serikali.
Baadhi ya wakulima waliofanikiwa kutumia zana za kisasa kutoka Zana Bora Limited waliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa mkombozi wao kwani wamefanikiwa kuongeza mashamba na kuvuna mazao mengi zaidi.




