Na Mwandishi wetu, Simanjiro.
KIONGOZI wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 Ismail Ussi amempongeza Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Development Foundation kwa kujenga shule ya sekondari ya wasichana ya Tukuta iliyopo Kata ya Terrat itakayowanufaisha wana jamii hasa wakifugaji.
Ussi amesema Toima ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, amefanya jambo jema kwa kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ya Tukuta itakayowanufaisha wasichana wa jamii ya eneo hilo.
“Mwenyekiti angekuwa na tamaa angefuja fedha hizo kwa ajili ya kujitafutia madaraka ila amekuwa muungwana kwa kujenga shule ya sekondari ya wasichana itakayowanufaisha watoto hao wa kike,” amesema Ussi.
Amesema Toima ni miongoni mwa watu wanaopaswa kuungwa mkono katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ili kusaidiana na Serikali katika kunufaisha jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Toima amesema shirika lake la ECLAT Development Foundation kwa kushirikiana na shirika la Ujerumani la Upendo Foundation ndiyo wamehusika kujenga shule hiyo watakayoikabidhi Serikalini.
Toima amesema shule hiyo itawasaidia mabinti wa jamii ya eneo hilo ya kifugaji na wengineo kupata elimu bora hivyo kuondokana na changamoto ya kukosa elimu.
“Tunatarajia ifikapo mwezi Agosti mwaka huu wa 2025 shule hii itakamilika kwa upande wa madarasa ili mabinti hao waanze kunufaika na elimu ya sekondari,” amesema Toima.
Mratibu wa ECLAT Development Foundation, Bakiri Angalia
Bakiri amesema mradi huo wa shule ya sekondari ya wasichana Tukuta imegharimu kiasi cha shilingi 4,692,120,000 ambapo shilingi 216,000,000 ni thamani ya ardhini iliyotolewa na kijiji na shilingi 4,476,120,000 ni fedha zilizotolewa na mdau wa maendeleo.
Amesema shirika hilo makao makuu yake yapo kijiji cha Emboreet wilayani Simanjiro na kwa kipindi cha miaka tisa limejenga miundombinu 55 ya shule za msingi nchini, shule mbili za sekondari na chuo cha ufundi cha VETA, kituo cha mafunzo na maendeleo kwa wanawake, chuo kimoja cha NACTE 1 (kwa malezi na makuzi ya waschana).
Amesema miradi yote hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za kitanzania bilioni 26.
Bakiri amesema mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi 4,692,120,000 ambapo shilingi 216,000,000 ni thamani ya ardhini iliyotolewa na kijiji na shilingi 4,476,120,000 ni fedha zilizotolewa na mdau wa maendeleo.
Amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana Tukuta ni uchimbaji wa kisima cha maji na usambazaji wa maji, ujenzi wa madarasa manne na ofisi mbili.
Bakiri amesema ujenzi wa bweni, vyoo vya matundu nane na ujenzi wa nyumba za walimu na uchimbaji wa kisima cha maji umekamilika.
Amesema malengo ya mradi ni shule hiyo kuwa na miundombinu bora ya kujifunzia kwa wasichana, kuwa ya bweni ili kupunguza kiwango cha wanafunzi kuacha shule na kuwa na mazingira bora ya kufundishia.
“Kuwa na usawa wa kielimu kwa wasichana na wavulana na kuboresha ufaulu wa wasichana katika kanda hii na kusaidia kufanikisha malengo ya kitaifa kuhusu usawa wa kijinsia katika elimu,” amesema Bakiri.