Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Masuala ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki na bajaji yamepewa uzito mpya kufuatia uzinduzi wa kilainishi kipya cha Caltex Ezy 4T Plus, kilichozinduliwa rasmi wilayani Temeke, Dar es Salaam, huku Jeshi la Polisi likitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa waendeshaji hao.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkuu wa Usalama Barabarani Chang’ombe, Reverent Nkyami, alitoa wito kwa waendesha bodaboda na bajaji kujifunza kwa kina sheria za usalama barabarani kabla ya kuanza kutoa huduma kwa umma.
“Changamoto kubwa ni vijana kuingia barabarani bila elimu sahihi. Wanajifunza mitaani kwa siku moja au mbili kisha wanaanza kubeba abiria, bila uelewa wa sheria wala stadi sahihi za udereva,” alisema Nkyami.
Nkyami alieleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na kampeni mbalimbali za elimu na oparesheni maalum ili kudhibiti ajali, ambapo kwa sasa pikipiki zimekuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi zinazogharimu maisha na mali.
Katika tukio hilo, kampuni ya Karimjee Value Chain Limited ilizindua kilainishi hicho kipya kilichotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa, chenye uwezo wa kuhimili hadi kilomita 5,000 bila kubadilishwa, hatua inayolenga kupunguza gharama za matengenezo na kuongeza ufanisi wa injini.
Mkuu wa Kitengo cha Vilainishi wa kampuni hiyo, Anam Mwemutsi, alisema bidhaa hiyo ni majibu ya changamoto sugu ya uchakachuaji wa vilainishi unaosababisha uharibifu mkubwa wa injini.
“Tumeleta bidhaa inayolenga kumpunguzia mzigo mmiliki wa pikipiki, huku tukihakikisha usalama wake barabarani hauko shakani kutokana na injini isiyo imara,” alisema Mwemutsi.
Kwa upande wake, Msemaji Msaidizi wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Msisiri, aliipongeza kampuni hiyo kwa kushughulikia moja kwa moja tatizo ambalo limekuwa likiwasumbua kwa muda mrefu.
“Hili si tu suluhisho la kiufundi bali pia ni msaada wa kiusalama. Tunapoboresha injini zetu, tunapunguza ajali, na hivyo kulinda maisha ya abiria na waendeshaji,” alisema Msisiri.
Kampeni hiyo ya usalama barabarani iliyozinduliwa sambamba na bidhaa hiyo mpya imeonesha umuhimu wa kushirikisha wadau wa sekta binafsi katika kukuza usalama wa vyombo vya usafiri nchini.