NA Mwandishi wetu,Kibamba
Wataalam Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wametakiwa kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa tiba ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kupunguza gharama za kukarabati vifaa hivyo pale vinapoharibika.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Tiba MNH-Mloganzila Dkt. Elineema Meda wakati wa kongamano la kitaaluma lilokutanisha wataalam wa kada mbalimbali wa hospitali hiyo.
Dkt. Meda ameongeza kuwa matumizi sahihi ya vifaa tiba yataendelea kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwakuwa wagonjwa watakuwa na uhakika wa kupata huduma wakati wowote bila kikwazo chochote kinachotokana na ubovu wa vifaa tiba.
Akitoa mada katika kongamano hilo, Mkuu wa Idara ya Vifaa Tiba Mhandisi Chacha Saidi amesema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2024/2025 idara yake imefanya matengenezo ya vifaa tiba 250, utambuzi wa vifaa tiba vilivyoharibika 286, ukaguzi wa vifaa 180 na utekelezaji wa matengenezo kinga kwa vifaa 60.
Aidha, Mhandisi Chacha ameongeza kuwa idara yake imeendelea kutoa mafunzo kwa watumiaji, kufunga vifaa tiba 18 na utatuzi wa changamoto mbalimbali 102 hatua iliyoboresha utendaji kazi na kuendelea kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.



