Shinyanga
Ikiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, Kamati ya Ukaguzi ya TARURA imetembelea Miradi minne ya ujenzi wa miundombinu ya barabara mkoani Shinyanga.
Katika Manispaa ya Shinyanga Kamati ilitembelea ujenzi wa barabara ya Old Shinyanga-Chibe-Negezi kiwango cha changarawe na ujenzi wa Kalavati na daraja la Mawe la Nin’ghwa katika barabara hiyo.
Vile vile kamati hiyo ilipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Kinyata-Karena yenye urefu wa Km 0.8 kwa kiwango cha lami inayojengwa Kata ya Kambarage katika Manispaa hiyo.
Pia, Kamati imetembelea Mradi wa uondoaji vikwazo wa ujenzi wa Daraja la seli sita linalojengwa katika barabara ya Magonzo-Shinyanga unaotekelezwa chini Mradi wa RISE pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara ya DED-DC Km 1.0 kwa kiwango cha lami Wilayani Kishapu.
Akielezea manufaa ya Miradi hiyo kiuchumi na kijamii, Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Avith Rugemalila ameieleza Kamati hiyo kuwa itarahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa ndani na nje ya Manispaa ya Shinyanga pamoja na Wilaya ya kishapu.
“Miradi hii pia itavutia biashara na uwekezaji katika Mkoa wetu na hatimaye kuongeza pato kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla” ameongeza Mhandisi Rugemalila
Naye, Paulo Izengo Mkazi wa Wilaya ya Kishapu ambaye ni bodaboda ameishukuru Serikali kwa kuwajengea barabara hiyo kwani mazingira ya biashara yao yamekuwa mazuri na sasa gharama za matengenezo ya bodaboda zimepungua na faida imeongezeka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi TARURA CPA. Ally Rashid amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kutembelea Miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, kusikia changamoto kutoka TARURA Mkoa wa Shinyanga pamoja na Wakandarasi.
“Tunazichukua changamoto zote na kuona namna gani tutashauri na pale ambapo mmefanya vizuri vile vile ni kitu cha kupongeza ingawa sio kitu cha kupongeza sana kwa sababu ni wajibu wenu vitu viende vizuri na ni sehemu ya uwajibikaji”. amefafanua CPA. Rashid.