Aliyekuwa beki wa kati wa Simba SC, Che Fondoh Malone, sasa ni mchezaji halali wa klabu ya USM Alger ya Algeria baada ya kufuzu vipimo vya afya na kusaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza akiwa jijini Algiers mara baada ya kuthibitishwa kuwa mchezaji mpya wa timu hiyo, beki huyo raia wa Cameroon amesema licha ya kuondoka Simba, bado anaamini klabu hiyo iko kwenye njia sahihi na iko karibu kufika kilele cha mafanikio makubwa chini ya Kocha Fadlu Davids.
“Soka ni safari yenye hatua tofauti,” alisema Che Malone na kuongeza. “Leo niko hapa Algeria, nikiwa na mwanzo mpya, lakini moyo wangu bado unaiheshimu Simba. Siwezi kuondoka bila kusema ukweli”
“Kocha Fadlu Davids anajenga kitu kikubwa. Nimekuwa naye, nimeona mbinu zake, namna anavyowasimamia wachezaji na ninayo imani Simba itafika nchi ya ahadi.”
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa USM Alger, mkataba wa uhamisho wa Malone kutoka Simba una kipengele kinachoiruhusu Simba kupata asilimia 15 ya ada yoyote endapo atauzwa kutokea hapo.
Che Malone ameondoka wakati Simba imeshusha tayari beki mwingine wa kati Rushine De Reuck (29) kutoka Mamelodi Sundowns kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza.