MUNICH: Winga wa Liverpool Luis Diaz amekamilisha uhamisho wa Euro milioni 65.5 kwenda kwa mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia amesaini mkataba wa miaka minne na klabu hiyo ya Ujerumani na kuhitimisha safari yake ya miaka yake mitatu na nusu katika viunga vya Anfield.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 hakuwa sehemu ya kikosi katika mechi ya Liverpool ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya AC Milan Jumamosi baada ya kushika kasi kwa tetesi juu ya mustakabali wake ndani ya Liverpool.
Wakiwa wamekataa ofa ya Bayern ya pauni milioni 58.6 mapema mwezi huu, Liverpool ilikubali ombi lililofuata lenye nyongeza ya pauni milioni 65.5 mwishoni mwa wiki na kumpa Diaz ruhusa ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na klabu hiyo.
“Nina furaha sana, ina maana kubwa kwangu kuwa sehemu ya FC Bayern. Ni moja ya klabu kubwa duniani. Nataka kuisaidia timu yangu mpya na aina yangu ya soka. Lengo langu ni kushinda kila taji linalowezekana tutafanyia kazi hilo kila siku kama timu.” alisema Diaz, ambaye atavaa jezi namba 14 katika klabu hiyo
Diaz alijiunga na Liverpool kutoka FC Porto kwa kitita cha pauni milioni 37 Januari mwaka 2022, na kufunga mabao 41 katika mechi 148 alizocheza Anfield.
Alishinda Kombe la FA na Kombe la EFL wakati wa msimu wake wa kwanza akiwa na Reds, na alikuwa sehemu ya timu iliyopoteza kwa Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2022. Diaz alikuwa msimu mzuri zaidi wa maisha yake soka Anfield msimu uliopita akifunga mabao 17 katika mashindano yote huku Liverpool ikishinda taji la Premier League.
The post Diaz ahamia Bundesliga first appeared on SpotiLEO.