DAR ES SALAAM: BONDIA nyota wa Tanzania, Mfaume Mfaume, ametoa kauli ya kuomba radhi kwa mashabiki wa ndondi nchini, akisema hakuridhishwa na kiwango chake kwenye pambano lake la hivi karibuni dhidi ya bondia Kudakwache Banda wa Malawi, licha ya kushinda kwa pointi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mfaume ameandika ujumbe mrefu wa kugusa moyo, akieleza sababu zilizopelekea kucheza chini ya kiwango na kutowaomba radhi mashabiki waliokuwa na matarajio makubwa.
“WaTanzania kwa ujumla, kwanza niwashukuru sana kwa sapoti yenu. Pili niwape pole kwa timu Mfaume kwa mchezo ambao hata mimi baada ya pambano nimelirudia raundi zote. Kweli nimeshinda kwa pointi lakini sikucheza vizuri kabisa nakiri,” ameandika Mfaume.
Katika maelezo yake, Mfaume amekiri kufanya makosa makubwa kwa kumdharau mpinzani wake kutoka Malawi, jambo ambalo liliathiri namna alivyoingia kwenye pambano hilo.
Pia, ameeleza namna alivyosumbuliwa na uzito mkubwa kabla ya pambano hilo, hali iliyomlazimu kupunguza kilo kwa haraka, akifosi kupigana kwenye uzito mkubwa zaidi huku akiwa hajafanya mazoezi ya kutosha kutokana na muda mrefu wa kutopigana.
Hata hivyo, bondia huyo amesema kwa sasa yuko salama kimwili na kiakili, na amewahakikishia mashabiki wake kuwa pambano lijalo litakuwa la furaha kwao.
The post Mfaume aomba radhi, asema alimdharau mpinzani wake first appeared on SpotiLEO.