DAR ES SALAAM: KIKOSI cha Simba kimepanga kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Police FC ya Kenya katika kilele cha tamasha la Simba Day litakalofanyika ndani ya Mwezi Agosti, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakuwa ya aina yake kwa kuwa itatoa nafasi kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kuwaona wachezaji wao wapya wakionesha uwezo wao kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki.
Licha ya Simba kutoweka wazi juu ya timu watakavyocheza nao siku hiyo, Kocha Mkuu wa Police FC, Etienne Ndairagije, ambaye aliwahi kuinoa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), amethibitisha kuwa wamepokea mwaliko rasmi kutoka Simba na tayari wameanza maandalizi kwa ajili ya mchezo huo wa kihistoria.
“Kulikuwa na mazungumzo, viongozi wameniambia niandae timu kwa ajili ya kucheza mchezo huo wa kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi,” amesema.
Ndairagije amesema watakuja na kikosi imara kuonesha ushindani mkubwa dhidi ya moja ya klabu bora ukanda wa Afrika Mashariki.
“Ni heshima kubwa kwetu kualikwa kwenye tukio kubwa kama Simba Day. Simba ni klabu kubwa na ina historia kubwa, tunakuja Tanzania kwa lengo la kushindana na si kushiriki tu,” amesema Ndairagije.
Simba Day imekuwa tukio kubwa na la kipekee katika kalenda ya soka Tanzania, ambapo kila mwaka huambatana na shamrashamra, burudani kutoka kwa wasanii na mechi ya kirafiki ya kimataifa safari hii, Police FC ya Kenya ndiyo watakaopambana na mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu
The post Simba kucheza na Kenya Police FC Simba Day first appeared on SpotiLEO.