Mbeya City imetuma maombi ya kumuhitaji mshambuliaji wa Simba, Valentino Mashaka baada ya nyota huyo kushindwa kupenya katika kikosi cha kwanza, mbele ya washambu liaji wenzake kikosini humo, Leonel Ateba na Steven Dese Mukwala.
.
Mashaka aliyejiunga na Simba Julai 5, 2024 akitokea Geita Gold, ameshindwa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha timu hiyo chini ya kocha Fadlu Davids, jambo linaloifanya Mbeya City kuanza kuiwinda saini yake kwa lengo la kuongeza nguvu.
.
Natambua katika mazungumzo yanayoendelea, mabosi wa Mbeya City wanamuhitaji nyota huyo kwa mkopo wa msimu mzima, ambapo Simba haina tatizo na suala hilo, ingawa kilichobakia ni kwa mchezaji wenyewe kufikia makubaliano binafsi.
.
Taarifa ambazo nimezipata zinaeleza mabosi wa Simba wanataka kumtoa Mashaka kwa mkopo kwenda timu itakayompa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwa lengo la kulinda kipaji chake, huku Mbeya City ikiwa ni sehemu sahihi kwake kwenda.
.
Mbali na Mashaka anayewaniwa na Mbeya City, nyota wengine pia waliosajiliwa hadi sasa na kikosi hicho ni mabeki wa kati, Ibrahim Ame aliyetoka Mashujaa, Kelvin Kingu Pemba aliyekuwa Tabora United na kiungo, Omary Chibada wa Kagera Sugar.