Mwenendo wa soka nchini Tanzania unaendelea kuwa wa kuvutia, hasa kutokana na mvutano wa maneno kati ya klabu mbili kongwe – Yanga SC na Simba SC.
Hali hii imechukua sura mpya baada ya msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, kuposti picha ya beki wa kushoto wa Taifa Stars, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, akiwa kwenye jezi ya timu ya taifa, akifuatisha na ujumbe wa maneno: “Mimi nimesha move on, Mimi nawewe basi.”
Ujumbe huo umeibua tafsiri nyingi mitandaoni, hasa ikizingatiwa kuwa Tshabalala kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kugoma kuongeza mkataba na Simba SC, aliyodumu nayo kwa muda mrefu.
Ingawa Simba walitaka kumbakiza, mazungumzo kati yao yalikwama kutokana na kutokubaliana kuhusu masuala ya kifedha na masharti ya mkataba mpya.
Wakati gumzo hilo likiwa bado halijapoa, Tshabalala aliibuka na kiwango bora katika mechi ya ufunguzi wa Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso, ambapo Stars walishinda mabao 2-0. Tshabalala alifunga bao la kuvutia huku penalti ikifungwa na Abdul Suleiman.
Kutokana na kiwango hicho, Ally Kamwe alitumia nafasi hiyo kuashiria kuwa Tshabalala tayari ameachana na Simba SC na yupo tayari kwa hatua mpya, ikielezwa huenda akajiunga na Yanga SC.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, mchezaji huyo yupo katika hatua za mwisho za mazungumzo na Yanga SC, ambapo ofa nono inayojumuisha mshahara mkubwa na dau la usajili inadaiwa kuwa imemvutia.
Hatua hii ni sehemu ya mikakati ya Yanga SC ya kuimarisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na mashindano ya kimataifa.