WASANII wawili maarufu kutoka Afrika — Cici kutoka Afrika Kusini na Mimi Mars kutoka Afrika Mashariki wameungana kwa mara ya kwanza katika kazi ya pamoja kupitia wimbo mpya wa mapenzi uitwao “Running”, uliomo kwenye albamu mpya ya Cici ya Busisiwe 2.0.
Wimbo huo, unaoelezewa kama simulizi ya roho mbili zinazotafuta uponyaji na matumaini kupitia mapenzi, unavuma kwa kasi kwenye majukwaa ya burudani Afrika Mashariki na Kusini. Kupitia sauti zao laini na ujumbe wa hisia, Cici na Mimi Mars wameibua mazungumzo mapya kuhusu aina ya mapenzi yanayojenga na kuponya.
“‘Running’ unahusu kuchagua upendo badala ya hofu,” anasema Cici. Naye Mimi Mars anaongeza kwa kusema, “Ni aina ya mapenzi ambayo hauyakimbii, bali unayakimbilia.”
Ushirikiano wao umeleta muunganiko wa kipekee wa ladha ya muziki wa Amapiano kutoka Afrika Kusini na Afro-R&B ya Afrika Mashariki, na kwa pamoja wamewasilisha sauti ya mwanamke wa Kiafrika kama chombo cha nguvu katika tasnia ya muziki.
Wimbo huu umedhihirisha jinsi muziki unavyoweza kuvuka mipaka ya kitaifa na kiutamaduni, na kuwaunganisha wasanii pamoja na mashabiki katika jukwaa moja la hisia na ubunifu.
Kwa sasa, ‘Running’ unapatikana kwenye majukwaa yote ya kidijitali ikiwemo Spotify, Apple Music, na Boomplay, na tayari umeanza kupenya kwenye chati mbalimbali barani Afrika, ukiashiria mafanikio makubwa kwa ushirikiano huu wa kuvutia.
The post Cici na Mimi Mars waungana first appeared on SpotiLEO.