WARSAW: MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya Poland Robert Lewandowski amerejea kwenye kikosi cha timu hiyo, baada ya mshambuliaji huyo wa Barcelona kujiondoa katika timu ya taifa kufuatia mzozo na kocha wake wa awali Michal Probierz uliotokana na kuvuliwa unahodha wa timu hiyo na kupewa Piotr Zielinski wa Inter Milan.
Kocha mpya wa kikosi hicho Jan Urban alichukua nafasi ya Michal Probierz, ambaye alijiuzulu mwezi Juni kufuatia mzozo huo na kuashiria ushindi kwa Lewandowski, nahodha na mfungaji bora wa muda wote wa Poland.
Poland inashika nafasi ya tatu katika kundi lao la kufuzu kwa Kombe la Dunia nyuma ya Finland na Uholanzi na Lewandowski anaonekana kuwa muhimu kwa matumaini yao ya kufuzu michuano ya Kombe la dunia la mwaka ujao.
“Nataka tuanze kambi ya mazoezi kwa utulivu. Robert Lewandowski atakuwa nahodha wa timu, na atakuwa nami katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu. Nimemteua Piotr Zielinski kuwa nahodha msaidizi na Jan Bednarek atakuwa nahodha wa tatu.” – Urban amesema katika taarifa yake.
Mchezo ujao wa Poland wa kufuzu Kombe la Dunia ni dhidi ya Uholanzi ugenini Septemba 4 kabla ya kuwakaribisha Finland siku tatu baadaye. Lewandowski, mwenye umri wa miaka 37, amefunga mabao 85 katika mechi 158 alizoichezea Poland.
The post Lewandowski arejeshwa kikosini Poland first appeared on SpotiLEO.