CAPE TOWN: TIMU ya Taifa ya Visiwa vidogo vya Cape Verde imeendelea kushika nafasi ya kwanza katika kundi lao la kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 baada ya ushindi wa ugenini usiku wa kuamkia leo, huku Algeria na Tunisia pia zikipiga hatu kuelekea kufuzu kwa fainali hizo za mwaka ujao nchini Marekani, Canada na Mexico.
Timu ya Cape Verde, ambayo hunufaika pakubwa na vipaji vya jamii za wahamiaji kutoka barani Ulaya, waliifunga Mauritius mabao 2-0 ugenini huku Jovane Cabral na Diney wakihakikisha taifa hilo linasalia kileleni mwa Kundi D wakiwa na pointi 16, moja mbele ya Cameroon, ambao pia walipata ushindi wa 3-0 dhidi ya Eswatini mjini Yaoundé.
Cameroon, ambao wana rekodi ya kufuzu mara nane fainali hizo za Kombe la Dunia mara nyingi kuliko taifa lingine lolote, walipata mabao matatu ya haraka haraka ndani ya dakika 28 za mwanzo lakini hawakuweza kuongeza na kutanua uongozi huo.
Ushindi wa Libya wa 1-0 ugenini nchini Angola, ambapo Ezzedine El Mariamy alifunga mapema kipindi cha pili, unawaweka katika nafasi ya tatu katika Kundi D wakiwa na pointi 11.
Cape Verde sasa wanakaribia kuweka historia kwa kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye Kombe la Dunia huku hali ikiwa si shwari kwa Angola, Eswatini na Mauritius ambao wapo kwenye hatari ya kuondoshwa.
Ni Timu itakayoshika nafasi ya kwanza pekee itafuzu moja kwa moja kwa michuano hiyo huku nafasi ya pili wakiwa na nafasi ya kucheza playoff kama ikiwa miongoni mwa timu nne zitakazomaliza nafasi ya pili kwa uwiano mzuri wa pointi.
The post Cape Verde yakataa unyonge kwa Cameroon first appeared on SpotiLEO.