DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba imezindua rasmi tawi jipya la VIP A Magomeni, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha mshikamaniko wa wanachama na mashabiki wake.
Katika uzinduzi huo uliofanyika Dar es Salaam Leo, Msemaji wa klabu hiyo Ahmed Ally amewahimiza mashabiki kuishi kwa kufuata miongozo ya timu hiyo.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Ahmed Ally, amewapongeza waanzilishi wa tawi hilo kwa hatua waliyochukua, akibainisha kuwa chanzo chake kilianza kama kikundi cha mashabiki waliokuwa wanakaa sehemu moja uwanjani.
“Niwapongeze kwa kufungua tawi hili, mwanzoni ilianza kama kikundi kukaa sehemu moja uwanjani baadaye wakaungana na kuanza mchakato wa kufungua tawi. Ni jambo la kupongeza, hongereni sana,” alisema Ahmed.
Alisisitiza umuhimu wa wanachama wa tawi hilo kuishi kwa kufuata miongozo ya Simba SC na kulinda chapa ya klabu hiyo.
“Kuanzia sasa mnatakiwa kuishi kwa kufata miongozo ya Simba Sports Club. Viongozi na wanachama wa VIP A mnatakiwa kuipambania chapa ya Simba Sports Club, sio kuisema vibaya. Kazi yenu ni kuisemea vizuri Simba,” aliongeza msemaji huyo.
Akizungumzia maandalizi ya Simba Day itakayofanyika Jumatano, Ahmed aliwataka wanachama kujitokeza kwa wingi na kusisitiza kuwa tiketi zilizotumika katika mchezo dhidi ya RS Berkane bado zitakuwa na umuhimu kwa waliokuwa na kadi za manunuzi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wanachama wa Simba, Hamisi Kissiwa, aliwataka wanachama wa VIP A Magomeni kushiriki kikamilifu katika kila tukio la Simba na kueleza kuwa klabu hiyo haina baya kwa mashabiki wake bali imejaa mazuri yanayohitaji kusherehekewa.
“Hakikisha kama tawi mnashiriki kila tukio la Simba. Simba haina baya, kila siku ina mazuri hivyo mjiandae kwa hilo. Jumatano tutakuwa na Simba Day, mjitokeze kwa wingi kusherehekea siku hii muhimu,” alisema Kissiwa.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wanachama na viongozi mbalimbali wa Simba SC, huku tawi hilo likiahidi kuunga mkono kila hatua ya maendeleo ya klabu.
The post Ahmed awataka mashabiki kufuata miongozo ya Simba first appeared on SpotiLEO.