BUENOS AIRES: NAHODHA wa timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi ameaga kwa staili ya kipekee kwa kuingia kambani mara mbili katika mechi yake ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia katika ardhi ya nyumbani wakati Argentina ilipoilaza Venezuela 3-0.
Mshindi huyo mara nane wa tuzo ya Ballon d’Or bado hajaonesha dalili ya lini anapanga kustaafu lakini ameweka wazi kuwa mechi dhidi ya Venezuela ni mechi yake ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia katika ardhi ya nyumbani Argentina.
Argentina, Mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, ambao tayari wamefuzu michuano ijayo nchini Marekani, Canada na Mexico waliudhibiti mchezo huo kuanzia mwanzo, na kutengeneza nafasi kupitia kwa Nicolas Tagliafico na Franco Mastantuono na kuzuiwa na kipa wa Venezuela Rafael Romo.
Messi alifunga bao la kwanza dakika ya 39, akiunganisha pasi ya Julian Alvarez kwenye shambulizi la kushtukiza na kupiga shuti kali na lililopiga kona ya juu kulia ya lango la Romo.
Argentina waliendeleza moto wao katika kipindi cha pili, huku Messi akisalia kitovu cha mashambulizi, lakini walilazimika kusubiri hadi dakika ya 76 kupata bao la pili, Nico Gonzalez akimimina mpira ambao ulifika kwa Lautaro Martinez aliyefunga kwa kichwa.
Dakika nne baadaye, Messi alimaliza mchezo huo kwa bao la tatu, akipokea asisti kutoka kwa Thiago Almada.
“Kumaliza hivi na watu wangu ndilo jambo ambalo nilitamani mara zote. Kwa miaka mingi nilijenga mapenzi na mashabiki wa Barcelona na ndoto yangu ilikuwa kuwa nayo hapa nchini kwangu pia.” – Messi mwenye hisia kali alisema baada ya mechi.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wake wa kustaafu, Messi ambaye ana rekodi ya mabao 36 katika mechi za kufuzu kwa Amerika Kusini, alisema: “Si kitu ninachokipenda, ninachokitaka au kutarajia. Lakini muda unaenda, na ni miaka mingi imepita.”
Timu ya taifa ya Argentina (Albiceleste) inaongoza msimamo wa ligi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 wakiwa na pointi 38 na watawavaa Ecuador Jumanne katika mechi yao ya mwisho ya kundi.
Tofauti na mashirikisho mengine Duniani, CONMEBOL inatumia mfumo wa ligi yenye jumla ya timu 10 na kila timu kucheza dhidi ya nyingine nyumbani na ugenini. Kwakuwa michuano ya mwaka ujao itahusisha timu 48, timu sita za juu zitafuzu moja kwa moja huku nafasi ya saba ikicheza playoff na timu nyingine kutoka shirikisho la soka Asia (AFC), shirikisho la Oceania (OFC) au shirikisho la soka Amerika kaskazini, kati na caribbean (CONCACAF).
The post Messi aaga kiania Argentina first appeared on SpotiLEO.